NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu Bunge Ajira Vijana na Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka viongozi wa Vyama vya watu wenye ulemavu kutokata tamaa ili kulitengenezea njia kundi hilo ili lifikie malengo ya kujiletea maendeleo.
Nderiananga ameyasema hayo leo Mjini Kibaha wakati wa maadhimisho ya siku ya Fimbo Nyeupe Kitaifa ambapo yamewashirikisha viongozi na wanachama wa Chama Cha Wasioona (TLB).
Nderiananga alisema kuwa watu wenye ulemavu wana uwezo mkubwa kama walivyo watu wanaoona na wanauwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na za kiuchumi.
Aidha amesema kuwa serikali imekopesha watu wenye ulemavu kiasi cha shilingi bilioni 12.9 hadi kufikia Agosti mwaka huu fedha zitokanazo na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kote nchini na fedha hizo zimeweza kuwanufaisha kundi hilo.
Naye Margareth Matonya mkurugenzi anayeshughulikia watu wenye mahitaji maalumu kutoka wizara hiyo alisema kuwa mwaka huu wametoa mafunzo kwa walimu na 1,373 wathibiti ubora 200 kwa lengo la kukagua miundombinu kama inafikika eneo la ujifunzaji na ufundishaji na wanaangalia walimu wanavyofundisha wanafunzi wenye ulemavu.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kibaha Sara Msafiri ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani alisema kuwa mkoa huo umejenga mabweni kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwenye Halmashauri Chalinze na Mkuranga.
Awali mwenyekiti wa Chama cha Wasioona TLB Omary Sultan alisema kuwa maadhimisho hayo ni kwa ajili ya kukaa na kutafakari masuala mbalimbali ya wanachama ili kujua changamoto na mafanikio na kujifunza masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi, kijamii, afya na masuala ya maendeleo.
0 Comments