Timu ya mpira wa miguu ya Iringa LIPULI imepokea vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 24 za kitanzania kutoka kwa kampuni ya Vunja Bei.
Vifaa hivyo vilipokelewa na mkuu wa wilaya Mohammed Moyo katika duka la nguo linalomilikiwa na Fred Ngajilo maarufu kama Vunja bei lililoko mitaa ya Uhindini mkoani Iringa
Wakati akipokea vifaa hivyo Moyo alisema anaushukuru uongozi wa maduka ya Vunja bei kwa upendo wao waliouonyesha kwa timu ya lipuli na kuwaomba wengine pia wajitokeze katika kudhamini timu hiyo ili iweze kupanda daraja na hatimaye kucheza ligi kuu.
''niwashukuru vunjabei kwa kuleta vifaa hivi, pia nitoe shukrani kwa uongozi wao kwa kutimiza ahadi waliyokuwa wameiweka maana sio kampuni zote zinaweza kutimiza kile ambacho watakuwa wamekiahidi ila nyinyi mmeweza na ukiangalia timu hii imeshuka daraja kwa sasa, hivyo naomba muendee na moyo huohuo wa kuisaidia timu hii'' alisema Moyo
Moyo alisema wao kama Serikali wanalifanyia kazi swala la wadhamini maana ndio limekuwa changamoto kubwa kwa timu hivyo watahakikisha wanazungumza na baadhi ya wadau ili waweze kuisaidia timu katika kila sekta ili iweze kupanda daraja na kucheza ligi kuu.
''timu hii inahitaji wafadhili wengi lakini sisi kama serikali tunalifanyia kazi, na wakati mwingine sio lazima kila siku uende na kujitokeza hadharani na kusema mimi nipo hapa naisaidia timu hapana maana timu ya lipuli ina heshima kubwa kwahiyo tunalifanyia kazi, tunatambua changamoto za lipuli zilizopelekea kushuka daraja, mimi na wadau tunalifanyia kazi pia kwa wale wote waliokuwa wanaisaidia lipuli mwanzo bado tunaongea nao ili waweze kuisaidia timu hii tena''
Kwa upande wake Meneja masoko wa Kampuni ya vunja bei Fadhili Ngajilo alisema kuwa mwaka jana walisaini mkataba wa miaka miwili na timu ya lipuli kwa ajili ya kuwapatia vifaa vya michezo ambapo kwa mwaka jana walitoa vifaa vyote vya timu kwa ajili ya kuchezea uwanjani pamoja na kufanyia mazoezi.
''tunathamini sana uwepo wa timu ya lipuli kwahiyo tumejitoa kwa miaka kadhaa kuisaidia timu na mwaka jana tulitoa vifaa na mwaka huu tutatoa vifaa vyote kwa ajili ya kuchezea uwanjani na kufanyia mazoezi. Mungu akipenda huko mbeleni tutafanya vizuri zaidi''
Fadhili alisema timu ya lipuli bado inauhitaji mkubwa wa msaada na kwa upande wa vunja bei wamewasaidia kwa kuwapa vifaa tu na kuwaomba wale wenye uwezo wa kuendelea kuipa ushirikiano timu kwa chochote basi wajitoze ili timu iweze kusonga mbele.
''sitaki kusema tulichotoa sisi ndio kikubwa sana kwamba kinajitosheleza, timu ya lipuli ina uhitaji mkubwa sana wa msaada, sisi tumetoa vifaa tu kwahiyo wale wenye uwezo wa kuisaidia timu ya lipuli kwa maana ya fedha ili timu hii iweze kuvuka na kurudi katika ligi kuu watakuwa wamefanya jambo jema na watakuwa wameungana na sisi.'' alisema Ngajilo





0 Comments