Mwaka 1991 nikiwa mwanafunzi huko Tambaza Sekondari nikiwa darasani alipita kijana mmoja ambaye kwa jina la utani alifahamika kama Puza, ndugu huyu alikuwa kijana mwenye nguvu sana na akiogopwa na kila mmoja wetu. Mara nyingi kama mtu akionewa na mwezake kama utamueleza kijana Puza alikuwa akimtafuta ndugu huyo muonezi na kumshikisha adabu, chamno ni kuondoa uonevu shuleni....ADELADIUS MAKWEGA_MBAGALA
Kijana huyo alikuwa na mwili uliojengeka, mrefu na hata kwenye sehemu ya kunyanyua vyuma vizito ya shuleni hapo yeye pekee ndiyo alikuwa akiweza kunyanyua vyuma vizito kuliko vyote. Siku hiyo nikiwa darasani huku mwalimu wa somo la Kifaransa akiendelea kutufundisha lugha hiyo.
“Jemapele Musa, Jemapele Adeladius.” Ikimaanisha jina langu Musa, Jina langu Adeladius. Huku tukifundishwa na tukijaribu kutamka maneno haya ya utambulisho ya lugha hiyo. Mara tulisikia kijana Puza akibisha hodi akiwa na mwenzake, mwalimu alitoka nje na kuwasikiliza wakamueleza jambo lao, mara mwalimu akarudi nao ndugu hawa wawili darasani.
Kijana Puza alikuwa anajiamini sana alitusalimu akasema jamani mimi leo kaka yenu nimeambatana na huyu mwezenu, alimtaja jina lake, yeye kwao ni Moshi, lakini alifaulu hapa Tambaza mwaka 1989 kuanza kidato cha kwanza, sasa yupo kidato cha pili lakini pahala alipokuwa anakaa kumetokea mgogoro baina ya huyo aliyekuwa anaishi na mwenza wake.
Jambo hili alielezwa mkuu wa shule Mwalimu Julius Mushi na akamsaidia akakaa bweni na kidato cha tano na sita ili kumsaidia kwa siku chache wakati uhamisho unashughulikiwa wizarani. Kwa hiyo nimeongea na mkuu wa shule ameeleza kuwa uhamisho umefika na kesho mwenzetu anaondoka kuhamia huko Old Mushi sekondari.
“Kwa heshima na taadhima nawaombeni, wadogo zangu tumchangia ndugu huyu fedha, ili zimsaidie aweze kuelekea huko na kununua vifaa kadhaa vya shuleni.”
Mara baada ya Puza kumaliza mchango ulichangishwa na huku Puza akishika kofia ambayo kila mmoja wetu alichangia. Wakati mchango huo unaanza tu ulianzishwa wimbo wa Toa ndugu na mtu ambaye sikumfahamu, huku mwalimu wa Kifaransa akicheka tu.
“Toa ndugu, toa ndugu, toa ndugu, ulichonayo wewee, bwana anakuona hadi moyoni mwako. Wiki nzima, Bwana Yesu amekulinda vema, sasa nawe ndugu ujifikirie…Toa ndugu, toa ndugu, ulichonacho wewe, Bwana anakuona hadi Moyoni mwako.”
Kweli mchango ulikusanywa na kofia ilijaa pesa naye Puza akamaliza kukusanya na kutushukuru wote, huku akimtania mwalimu wetu wa somo la Kifaransa mbona hajachangia? Kweli mwalimu alitoa noti ya shilingi 200 ikaweka katika kofia hiyo na Puza akatoka nje.
Kweli yule kijana kumbe alikuwa akikaa kwa shemeji yake kukatokea mgogoro wa wapendanao, mke na mume wakaachana, dada akarudi Moshi kwa hiyo hakukuwa na namna na ya mwanafunzi huyu tuliyemchangia kusoma Dar es Salaam kubwa lilikuwa kupata uhamisho kwa shule za bweni huko Moshi ili aweze kusoma vizuri.
Tukio hili nimelikumbuka kwa sababu moja kubwa kuwa kwa siku ya jana niliwasiliana na ndugu yangu mmoja ambaye ambaye sijawasiliana naye kwa muda. Nilipowasiliana naye aliniambia kuwa kwa sasa haelewi kabisa mambo yanavyokwenda kwani alijaribu kuhama huko alipo lakini likagonga mwamba. Sasa anasema kuwa amebakiwa na matumaini ya yeye kuhamia Zanzibar.
Nikamuuliza unasemaje? Akasema anataka kuhamia Zanzibar.
Nikamuuliza kaka jamaa wamekunyima uhamisho wa kuhama mkoa mwingine ambapo unapita kwa barabara ya kuvuka milima na mito tu, watawezaje kukupa uhamisho wa kuvuka bahari? Ndugu huyu alinjibu kuwa kuna mkubwa mmoja anamfahamu kwa kuwa aliwahi kuishi na dada yake na kuzaa naye watoto basi atamfuata na kumlilia angalau kumueleza yanayomsibu hili akatulize akili kidogo huko Zanzibar.
Nilimpongeze sana kwa uamuzi huo kwa kuwa hakutaka kwenda nje ya Tanzania /kuukana urai bali yeye anakwenda Zanzibar angalua akapumzike maana mambo mengi yanamsibu. Nikamwambia pengine jamaa (shemeji yake) hawezi kukuelewa kabisa kwa kuwa mapenzi na dada yako yalishaisha. Ndugu huyu akajibu ni kweli lakini amezaa naye watoto, watoto wake ni wajomba zake hawawezi kufurahi kumuona mjomba anateseka, alisema. Hapo ndipo nikakikumbuka kisa hicho cha Puza na kijana wa Kichaga aliyekuwa akiishi kwa shemeji yake.
Nikamuuliza huyu ndugu yangu aliyekunyima kwenda mkoa mwingine anaweza akagoma kukupa ruhusa ya wewe kwenda Zanzibar akasema kuwa kama unataka kwenda huko basi nenda ila kazi yetu tuachie, hilo litakuwaje? Ndugu yangu huyu akasema tuombe Mungu kwani kila jambo lina arubaini yake iwe nzuri ama mbaya, arubaini ipo.
“Maana huku mie simjui mtu, siasa zenyewe za kujuana kaka, huyu wa fulani, huyu wa fulani, huyu hatufai ni wafulani. Mambo yenyewe kujuana, ngoja na mimi niende kwa anayenijua. Ningekuwa mtoto wa Bwenyenye ningekula urithi wa baba yangu lakini wapi, nimejaa ufukara.”
Nikiwa nazungumza naye ndugu huyu na mimi nikapata picha kumbe watu siku hizi wanakwenda Zanzibar kuna neema gani huko? Mambo yenyewe kujuana, Si bure na mimi hamu ikanijia. Lakini Mwana wa Makwega, pangu pakavu tia mchuzi namjua nani huko Zanzibar? Sina shemeji Mzanzibari, maana dada zangu hawavai ushungi wala baibui, sina mjomba wala ami kwa maana wajomba na ami zangu wa msalaba. Nilifikiri kwa muda kidogo likanijia wazo kuwa na mie namfahamu Zena Said ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, nitamlilia anitafutie kichaka cha kujificha huko Zanzibar.(haya yote niliyafikiri kimyakimya )
Ndugu yangu huyu niliyekuwa nazungumza naye alisema yeye hatompigia simu shemeji yake huyu bali atafunga safari hadi huko kimyakimya maana simu zinaweza kuharibu mambo.na mimi nikasema kimoyomoyo kuwa simpigii simu Dada Zena Said nitamfuata huko kimyakimya wakati ndugu yangu huyu anamfuata shemeji yake na mie nyuma nyuma hadi kwa Dada Zena Said.
Kimoyo moyo nikasema lakini kama siye wa bara wote tukihamia Zanzibar kile kisiwa si kitazama? Heri wa visiwani kukimbilia bara ambayo hapo awali ilikuwa desturi lakini hili la bara kukimbilia Zanzibar hapo tunakwenda kukizamisha kisiwa. Hakiwezi kuzama(Nikijijibu), kama kikizama Mungu kapenda hilo kutokea, kwani njaa zangu ndizo zinazonifanya nihangaike na atafutaye hachoki akichoka amepata.
Nilijiuliza swali je huyu ndugu shemeji yake na mimi Dada Zena tukipatiwa hicho kichaka cha kujificha, je hawa ndugu wakiondoka Zanzibar itakuwaje? Isije ikawa kama ile simulizi ya Puza na kijana wa Kichaga. Lakini nikajitia moyo, siku zitakuwa zimeshasonga, kwani duniani tunaishi milele? Nikikaa Zanzibar mwaka mmoja nitakuwa Mzanzibari Mkaazi mambo yatakuwa swari. Maisha yatasonga.
Najiandaa na mie kwenda Zanzibar kutafuta kichaka cha kuficha kwa maana natambua Dada Zena Said atanipokea na kusikiliza shida yangu kubwa na hilo la kupata kichaka cha kujificha maana Dada Zena Said wakati akifanya kazi bara alikuwa anaishi Mbagala alikuwa ni jirani yangu.
Makwadeladius @gmail.com
0717649257
0 Comments