BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limefuta matokeo ya mitihani ya nadharia kwa masomo yote ya programu ya utabibu ngazi ya tano (NTA Level 5). mwandishi wa matukio daima Hamida Ramadhani anaripoti kutokea Dodoma
Mganga, Mkuu wa serikali Dk. Aifello Sichalwe, alibainisha hayo jana jijini Dodoma wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kuvuja kwa mitihani ya utabibu.
Alisema, hatua hiyo imefikiwa baada ya kamati ya uchunguzi iliyoundwa kuwasilisha taarifa ambayo imethibitisha kuwapo kwa udanganyifu kwenye baadhi ya vyuo vilivyochunguzwa kupitia namba za simu za wanafunzi.
“Mtihani wa muhura wa pili kwa mwaka wa masomo 2020/2021 ilifanyika kitaifa kuanzia tarehe 16 Agosti, 2021 hadi Septemba 30, 2021 siku ya mwisho ya ufanyaji wa mitihani ya nadharia wizara ilipokea taarifa ya kuwapo kwa viashiria vya kuvuja kwa mitihanbi hiyo, hivyo kulazimika kuunda kamati ya uchunguzi iliyojumuisha wataalamu kutoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama”alisema Dkt, Sichalwe
Alisema kamati hiyo imefanya uchunguzi kuanzia Septemba 6, 2021 hadi Oktoba 17, 2021 ilipowasilisha taarifa ya awali katika uchunguzi huo.
“Kamati imebaini kwamba mitihani ya mwaka wa pili (NTA LEVEL 5) ya progaramu ya utabibu ilivuja lakini mitihani ya programu zingine zote haikuvuja”alisema
Aidha, alisema wakati wa uchunguzi kamati ilibaini mitihani hiyo ilisambazwa kupitia mitandao ya kijamii na kuonekana kwenye baadhi ya namba za simu za wanafunzi ambapo wanafunzi hao walipohojiwa walikiri kupata mitihani hiyo kupitia makundi ya mitandao ya kijamii yaliyoanzishwa na wanafunzi hao kwa ajili ya kujadiliana.
“Kamati ya uchunguzi imewasilisha taarifa ya uchunguzi ambayo imethibitisha kuwapo kwa udanganyifu kwenye baadhi ya vyuo vilivyochunguzwa kupitia namba za simu za wanafunzi, uchunguzi unaendelea ili kuwabaini watu, vyuo, taasisi zingine zilizo jihusisha na udanganyifu huo”alisema
Hata hivyo taarifa ya uchunguzi huo iliwasilishwa kwenye Baraza la taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) Oktoba 24, 2021 kwa ajili ya maamuzi kwani ndicho chombo cha kisheria chenye mamlaka na vyuo vya elimu ya kati nchini.
“Wizara imesikitishwa na tukio hilo na itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kukamilisha uchunguzi na kuwachukulia hatua wale wote walioshiriki kufanya udanganyifu”alisisitiza
Dkt, Sichalwe aliwataka wanafunzi wa vyuo kuzingatia masomo na kutojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu kwani vina madhara makubwa kwao na kwa jamii.
“Mtaalamu wa afya alijipatia sifa kwa njia ya udanganyifu ni hatari kwa afya za wananchi, tunaomba wananchi waendelee kuwa watulivu na waiamini serikali yao kuwa ipo makini na itatumia jitihada zote kulinda usalama wao”alisisitiza Dkt, Sichalwe
0 Comments