KATIKA kuadhimisha Miaka 60 ya UHURU wa Taifa la Tanzania Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye anafanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kushiriki katika ujenzi wa madarasa na miundombinu mbalimbali kama sehemu ya kuwahamasisha wananchi kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuendeleza maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania tangu ipate Uhuru. mwandishi wa matukio daima Editha Karlo anaripoti kutokea Kigoma
Andengenye aliwasisitiza wananchi wa kijiji cha Kagondo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita ambazo ni mwendelezo wa maono ya viongozi wa asasi wa Taifa la Tanzania.
Aliwakumbusha kuwa Taifa la Tanzania limejengwa kwa misingi ya umoja mshikamano na amani, hivyo tunapoelekea maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania kuna mengi yamefanyika ambayo twapaswa kumshukuru Mungu kwa tulipofikia.
Alisema hakuna anayeweza kubisha kwa kutumia historia na ya kushuhudia tangu uhuru Tanzania imeendelea sana katika nyanja na sekta zote zinazomgusa binadamu.
"Tunajivunia maendeleo ya elimu, Afya, miundombinu ya usafiri na usafirishaji pamoja na huduma nyingine za kijamii, kwani sote ni mashahidi tunaona namna viongozi wetu wakuu wa nchi wanavyoendelea kudumisha na kuziishi ndoto za waasisi wa Taifa hili kwa kudumisha amani na mshikamano" alisema Andengenye
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Izack Mwakisu aliwataka wananchi kushirikiana na serikali katika kuchangia miradi mbalimbali ili maendeleo yaweze kupatikana kwa wakati.
"Serikali yetu ya awamu ya sita inafanya jitihada kubwa sana kuleta maendeleo kwa wananchi wake hivyo hatuna budi kuiunga mkono na sisi kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo"alisema Kanali Mwakisu
Katia ziara yake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma alitembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali na Wadau wa Maendeleo katika Mkoa wa Kigoma.
0 Comments