Na Abubakari W Kafumba, UAE
Kamishna Jenerali Mhe. Balozi Mohammed Mtonga na Bi. Getrude Ng'wesheni kutoka TanTrade ambaye ndio Mkurugenzi wa Banda la Tanzania katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai leo tarehe 10 November, 2021 wamemkaribisha Kamishna Jenerali wa Banda la Marekani Bw. Robert Clark katika banda la Tanzania akiongozana na ujumbe wake mfupi kutoka banda la Marekani.
Bw. Clark amefurahishwa mno na ushiriki wa Tanzania kwenye maonesho haya ya Dunia ya Expo 2020 Dubai kwa kuwa anaifahamu vema Tanzania ilivyo barikiwa na rasimali za kipekee ambazo nchi nyingine ulimwenguni hawana. Ameeleza kuwa Tanzania iko katika nafasi nzuri zaidi ya kufaidika na ushiriki huu hasa katika uwekezaji kwenye sekta mbalimbali.
Bw. Clark alisema, “Mkusanyiko huu wa nchi 192 ni mkubwa sana na kupitia fursa hii mnaweza sana kupiga hatua ya kimaendeleo kwa kukutanishwa na wawekezaji wa uhakika wenye nia ya kuwekeza Zaidi kwenye sekta mbaimbali”.
Kutokana na uhusiano endelevu mzuri baina ya Tanzania na Marekani na kuridhishwa na hatua ya kimaendeleo na rasilimali muhimu zinazoweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, Kamishna Jenerali wa Banda la Marekani Bw. Clark amekubali kuiunganisha Tanzania na wawekezaji mbalimbali walio kwenye sekta za Madini, Utalii na Nishati.
Kwa upande wa uwekezaji kwenye madini Bw. Clark ameahidi kuiunganisha Tanzania na mfanyabiashara wa madini ya Cobalt ambayo hutumika sana kama malighafi na viwanda vya kutengeneza betri, hivyo ni fursa ya kupata soko la uhakika kwa wachimbaji wa madini ya Cobalt Tanzania.
Aidha, kwa upande wa Sekta ya Utalii Bw. Clark ameeleza kuwa kuna fursa kubwa kwa Tanzania kupata wawekezaji kwa upande wa Hoteli za Kitalii. Hivyo katika kuunga mkono hili ameeleza kuwa mmiliki wa Hoteli ya Kimataifa ya nyota tano ya Marriot Hotel anatarajia kuja kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai, hivyo ameahidi kumkutanisha na Sekta ya Utalii Tanzania ili kuangalia uwezekano wa namna nzuri ya kushirikiana na Tanzania katika kuwekeza kwenye Hoteli za Kitalii.
Mbali na hapo, Bw. Clark alisema kuwa utalii ni sehemu ya maisha yake baada ya kuona picha ya Mlima Kilimanjaro iliyo kwenye banda la Tanzania. Aliendelea kueleza kwamba yeye na wenzake waliwahi kwenda Tanzania kwa nia ya kutalii na kupanda Mlima Kilimanjaro. Kwake hii ilimkumbusha sana ukarimu wa Watanzania na upekee wa rasilimali zilizopo Tanzania. Ameahidi kurudi tena Tanzania na kuendelea kutalii kwa sababu bado kuna mengi ya kwenda kufurahia.
Vilevile, alipata nafasi ya kuona mradi mkubwa wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) ambapo ameweka wazi kuwa mradi huo utakapokamilika utaleta fursa ya kufanya uwekezaji mkubwa hususan katika Teknolojia. Amesema kuwa huko mbeleni Tanzania inaweza kufaidika na wawekezaji kwenye TEHAMA kama vile Google na Amazon.





0 Comments