Kombe la dunia 2022: Tanzania, Uganda matumaini yafifia kufuzu hatua inayofuata?
Hatua ya pili ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka ujao itafikia kilele chake wiki ijayo, kwa michezo itakayopigwa kati ya Alhamisi na Jumanne ijayo. Tanzania imepoteza mchezo wake nyumbani dhidi ya DRC kwa kufungwa mabao 3-0 na kupoteza matumaini ya kufuzu fainali hizo licha ya kuwa kabla ya mchezo huu, ilikuwa inaongoza kundi lake. Uganda imekwenda sare ya 1-1 na ndugu zao Kenya.
Ethiopia imeenda sare ya 1-1 na wakali wa soka la Afrika, Ghana katika michezo ambayo imepigwa mapema leo. Tanzania imesalia na alama zake 7, DRC ikiwa na alama 8. Ili Tanzania ifuzu hatua inayofuata inapaswa kushinda mechi yake ya ugenini dhidi ya Madagascar, na kuomba angalau sare ya 0-0 kati ya DRC na Benini, ambayo mchezo wake dhidi ya Madagascar inapaswa kufungwa. Ni mtihani mkubwa na hesabu zinazowezekana licha ya ugumu wake katika halihalisi.
Kutoka ukanda ya Afrika, timu nane zinatazamiwa kuungana na mataifa ya Morocco na Senegal katika mechi za mchujo za mikondo miwili mwezi Machi mwakani, wakati wawakilishi watano wa bara la Afrika katika fainali za kombe la dunia huko Qatar watakapojulikana.
Huku wachezaji kadhaa wakiwa nje ya uwanja kutokana na majeraha, mbali na Tanzania na Uganda, BBC imekuwa ikichunguza kwa undani ni nani anaweza kuungana na Wamorocco na Wasenegali ambao tayari wameshafuzu.
Timu zilizofuzu
Morocco, chini ya nyota wake anayekipiga Wolves, Romain Saiss na Senegal yenye mkali Sadio Mane wanaweza kupumua kwa urahisi baada ya kuvuka hatua ya awali ya makundi kukiwa na michezo miwili.
Mataifa mengine manane pekee wa kundi ndio watakaojiunga nao katika mchujo.
Mataifa yaliyo karibu kufuzu
Baada ya sare ya leo ya Ghana dhidi ya Ethiopia, inaipa nafasi kubwa Afrika Kusini kutinga hatua inayofuata, iwapo itashinda katika mchezo wake dhidi ya timu dhaifu kwenye kundi hilo ya Zimbabwe. Afrika Kusini imesalia na michezo miwili ikiwa na alama 10, ikiongoza kundi hilo, huku Ghana ikisalia na alama 10 na mchezo mmoja. Misri chini ya mkali Mohamed Salah ina pointi nne dhidi ya wapinzani wake wa karibu Libya baada ya kushinda mechi mbili mfululizo dhidi ya majirani zao hao wa kaskazini mwa Afrika mwezi uliopita.
Mafarao wanajua ushindi mmoja kati ya mechi zao mbili zilizosalia dhidi ya Angola na Gabon utawapeleka hadi hatua ya tatu na ya mwisho ya kufuzu, wakipania kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo.
Hata hivyo, kikosi cha Libya bado kinaweza kufuzu iwapo kitashinda michezo yake miwili iliyosalia na kuiombea Misri kupoteza katika michezo yake miwili iliyosalia.
Tunisia wanaongoza kwa alama tatu dhidi ya Equatorial Guinea katika Kundi B, wataweza kufuzu iwapo watashinda ugenini dhidi ya Waafrika magharibi katika mchezo wa tano wa timu hiyo kwenye kundi lake.
Kwa vile Tunisia wana uwiano mzuri wa mabao, vijana wa Mondher Kbaier bado wanaweza kuongoza kundi hata wakipoteza mchezo huo.
Ushindani mkali kwa baadhi ya makundi
Matokeo ya mwezi Oktoba yameacha makundi kadhaa yakiwa yamejiweka sawa, huku timu sita zitakazofuzu itabidi zisubiri mpaka mechi ya mwisho ya sita ya kundi
Katika Kundi A, mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika Algeria, wakiongozwa na Riyad Mahrez wa Manchester City na ambao hawajafungwa katika mechi 31, wako mbele ya Burkina Faso kwa tofauti ya mabao pekee, huku nchi hizo mbili zikitarajiwa kukutana katika mchezo wa mwisho baada ya kutoka Algeria kumenyana na Djibouti na Niger kukutana na Burkina Faso.
Ivory Coast wako mbele ya Cameroon kwa alama moja katika Kundi D. Ikiwa nchi zote mbili zitashinda katika mechi zao za mwishoni mwa wiki, wenyeji Ivory Coast wakiwakaribisha Msumbiji nchini Benin na Cameroon wakimenyana na Malawi nchini Afrika Kusini, Indomitable Lions watahitaji kuwafunga Tembo nyumbani ili kusonga mbele. .
Mshambuliaji wa Ivory Coast 'Tembo' mwenye uzoefu Gervinho atakuwa nje kwa sababu ya jeraha linalomsumbua kwa muda mrefu, huku nyota wa Bayern Munich Eric Maxim Choupo-Moting akiripotiwa kukosa mchezo ujao wa Cameroon baada ya kukutana na mtu ambaye alipimwa na kukutwa na Covid-19.
Kipa wa Ajax Andre Onana pia anaweza kucheza mechi yake ya kwanza kwa Indomitable Lions baada ya mwaka mmoja, akiwa amekaa nje kwa muda mwingi wa 2021 kwa sababu ya marufuku ya kutumia dawa za kusisimua misuli.
Maswahiba nahodha Ivory Coast Serge Aurier na mwenzake wa Vincent Aboubakar wanatarajiwa kuvaana uso kwa uso katika mchezo wa mwisho ambao huenda ukampata atakayefuzu kutoka kundi lao
Nigeria wako alama mbili mbele ya Cape Verde katika Kundi C baada ya Super Eagles kupokea kichapo cha kushangaza nyumbani dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Nigeria, ambayo imemrejesha mshambuliaji wa zamani wa Manchester United Odion Ighalo ambaye alistaafu michezo ya kimataifa, itacheza na Liberia nchini Morocco na Cape Verde watawakaribisha CAR kabla ya Super Eagles kuwakaribisha wenyeji hao katika mchezo wa mwisho wa hatua hiyo ya makundi.
Mali na Uganda hazijapoteza mchezo hata mmoja, huku Mali wakiwa mbele ya 'The Cranes' kwa alama 2 kwenye Kundi E. Uganda ina nafasi ya kufuzu ikishinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Mali na kuiombea Mali ipoteze dhidi ya Rwanda.
Tanzania imepoteza matumaini kiasi baada ya kipigo kutoka kwa DRC lakini Benini sasa matumaini yamesalia mikononi mwao ikicheza na Madagascar.
Wanaokaribia kuaga mashindano
Zambia (Kundi B), Jamhuri ya Afrika ya Kati (Kundi C), Gabon ya Pierre-Emerick Aubameyang (Kundi F) na Madagascar (Kundi J) bado wanaweza kuingia hatua inayofuata kwa hesabu za kawaida, lakini hatima zao haziko mikononi mwao, lazima, wategemee matokeo ya mechi zingine kwenye makundi yao.
Mataifa hayo matatu yanahitaji kushinda michezo yao miwili iliyosalia na kutumaini matokeo mengine yatawapa faida wao, pamoja na tofauti ya mabao.
Timu zilizotupwa nje
Mpaka sasa, timu 17 zimeondolewa kwenye mbio za kutafuta timu 10 za kuingia hatua ya mwisho ya kutafuta timu 5 za kuiwakilisha Afrika kwenye fainali za kombe la dunia.
Angola na Togo, ambazo zote zilifuzu katika fainali za Kombe la Dunia la 2006, ni miongoni mwa nchi ambazo haziwezi tena kufika fainali za mwaka ujao huko Qatari.
Kongo, Djibouti, Ethiopia, Guinea, Guinea-Bissau, Liberia, Kenya, Malawi, Mauritania, Msumbiji, Namibia, Niger, Rwanda, Sudan na Zimbabwe zote zilitupwa nje mwezi uliopita.CHANZO BBC
0 Comments