Mkoa wa Iringa umepongezwa kwa uchapaji kazi mzuri wa ujenzi wa taifa uliotukuka kwa kupitia kilimo cha vyakula mbalimbali hapa nchini Tanzania.
Hayo yalisemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari mkoani Iringa na kusema kuwa mkoa huu ni moja kati ya mikoa sita inayotegemewa kwa chakula hapa nchini na kuongeza kuwa mkoa huu unazalisha mahindi, maharage, mchele, viazi, ngano, njegere, karanga, kunde, ndizi, ulezi na pia maziwa .
Pia alizitaja takwimu mbalimbali za uzalishaji wa chakula kwa mwaka ikilinganishwa na mahitaji yake ambapo alisema tani 1,173,554 za chakula zinazalishwa kwa mwaka, huku mahitaji yake ni tani 703,206 zinazotosheleza wananchi 1,149,481.
''mkoa wa Iringa msimu uliopita umezalisha ziada ya tani 470,348 za mazao ya chakula hivyo kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea kuhakikisha inaleta fedha kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika mkoa huu kupitia bajeti yake ya mwaka huu wa fedha 2021/2022 shilingi Bilioni 211.701 zitakuja hapa, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 61 zitaelekezwa kwenye maendeleo, na tayari kwa mwaka huu wa fedha ulionza julai mpaka oktoba tumeshaleta shilingi bilioni 21 ndani ya mkoa huu wa Iringa''
Hata hivyo Msigwa alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Samia Suluhu anaupenda mkoa huu na tangu aingie madarakani tayari ameshaleta jumla ya shilingi bilioni 36 na milioni 210 kwa ajili ya kuendeleza na kuanzisha miradi mipya ya maendeleo kwa watu wa mkoa huu.
0 Comments