Header Ads Widget

FEDHA ZA KUINUA UCHUMI NA KUPAMBANA NA UVIKO KULETA NEEMA SEKTA YA ELIMU VUNJO.

Mnamo Oktoba 10 mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alizindua Mpango wa Serikali wa Kuinua Uchumi na kukabiliana na janga la Korona, UVIKO -19 wenye thamani ya shilingi trilioni 3.62 katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma. mwandishi wa matukio daima Gift Mongi anaripoti kutokea Vunjo

Wakati wa uzinduzi wa mpango  huo, Rais Samia aliitaka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na taasisi nyingine zitakazonufaika na fedha za mkopo wa Shilingi trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (International Monetaruy Fund-IMF) kuhakikisha zinatumika katika malengo yaliyokusudiwa.

Rais Samia alibainisha kuwa fedha hizo  za mkopo wa masharti nafuu kutoka IMF zitatumika katika kutekeleza Miradi ya Maendeleo ikiwemo kuboresha huduma za jamii katika sekta ya Afya, Elimu, Utalii na Maji.

Rais aliitaka sekta binafsi kutumia fursa hiyo kwa kuzalisha bidhaa zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo mfano uzalishaji wa saruji, mabati na nondo ili kusiwe na sababu ya kuchelewa kutumia fedha hizo.

Aidha  aliagiza miradi hiyo itekelezwe na wakandarasi wazawa ili fedha hizo ziendelee kubaki na kuzunguka katika uchumi wetu na kuwataka waweze kuwajibika kwa kufanya kazi kwa ubora, umakini na ufanisi.

Katika mpango huo ambao unatakiwa kutekelezwa ndani ya miezi 9, Rais Samia alitaka kutumika kwa utaratibu wa manunuzi wa (single source) ili kupunguza urasimu katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa miradi hiyo.

Katika jimbo la Vunjo tayari zimeshapokelewa fedha kiasi cha shilingi milioni 640 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vipatavyo 32 kwenye kata 8 ndani ya jimbo hilo.

"Napenda kuwajulisha wananchi wa Vunjo kupitia halmashauri ya Moshi kuwa tumepata fedha kwa ajili ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya uviko 19 kiasi cha milioni 640 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 32 katika jimbo hili" alisema Dkt Charles Kimei Mbunge wa Vunjo

Kwa mujibu wa Dkt Kimei ni kuwa jumla ya shule 11 kwenye kata 8 zimenufaika  katika mgawanyo huo ambapo  kata ya  Kahe Magharibi  vyumba vya madarasa 7 vinaenda kujengwa shule ya sekondari Mangoto ambavyo vitagharimu milioni 140 na Kahe Mashariki ni vyumba 04  katika shule ya sekondari Ghona ambapo milioni 80 zimetengwa.

Alisema pia fedha hizo zitajenga vyumba 03 vya madarasa katika shule ya sekondari Mrereni iliyopo katika kata ya Kilema kusini ambapo vitagharimu jumla ya milioni 60.

"Katika kata ya Kirua Vunjo Kusini shule ya sekondari Mashingia imepata mgao wa vyumba vitatu ambavyo ni sawa na milioni 60 pamoja na sekondari ya Uparo chumba kimoja ambapo ni Tsh 20Ml"Alisema

Dkt Kimei alisema shule ya sekondari Himo imepata vyumba vinne ambapo ni sawa na milioni 80 pamoja na Mieresini sekondari vyumba vinne sambamba na Lyakirimu iliyopo kata ya Mwika Kaskazini iliyopata vyumba viwili.

Mgao huo pia ulihusisha chumba kimoja kilichopo sekondari ya Makomu kata ya Marangu Magharibi na sekondari ya Mlang'a ambapo kwa ujumla wake ni milioni 40 huku shule ya sekondari Rasesa iliyopo kata ya Marangu Mashariki ikiambulia vyumba viwili vyenye thamani ya milioni 40.

Diwani wa kata ya Mwika Kaskazini Samwel Shao alisema kupatikana kwa mgao wa vyumba hivyo katika shule ya sekondari Lyakirimu utaenda kusaidia kutokana na kuwa na uhaba wa vyumba vya madarasa

"Tunaishukuru serikali kwa kutukumbuka katika mgawanyo huu wa kitaifa ni rai yangu wasimamizi wakahakikishe kuwa ujenzi huo unaenda kukamilika kwa wakati ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kutimia"alisema Shao

Diwani wa kata ya Makuyuni Dickson Tarimo alisema kata yake ambayo ni wanufaika kwa kupata vyumba nane vya madarasa sio haba kwani vitaenda kupunguza adha ya msongamano katika shule hizo kama sio kuumaliza kabisa 

Alisema atahakikisha kuwa karibu na kamati ya ujenzi ya shule ili majengo hayo yajengwe kwa muda na kiwango ili kusijekuwa na matumizi mabaya ya fedha hizo ambazo pia Rais Samia Suluhu Hassan alishazitolea maelekezo.

"Rais akishasema kitu huku kwetu ni utekelezaji tu ila niwahakikishie yu ujenzi unaenda kufanyika kwa viwango na muda uliopangwa maana hakuna jambo linalokwamisha tena hapa"alisema

Diwani wa Marangu Mashariki Jones Mawalla alisema msaada huo umekuja muda muafaka kutokana na uhitaji uliokuwepo shuleni hapo kwa kipindi kirefu na kuwa adha iliyokuwa sasa inaenda kufika mwisho

"Shule ya Rasesa ilitokana na Vijiji vitatu yaani Rauya,Sembeti na Samanga hivyo ina wanafunzi wengi kutoka vijiji hivyo na maeneo jirani hivyo hivi vyumba viwili vitaenda kutusogeza mbele kwa kiwango fulani"alisema

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI