Header Ads Widget

BASHUNGWA AIPONGEZA NBC NA RT KWA KUTOKOMEZA SARATANI NCHINI

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Innocent Bashungwa aliipongeza Benki ya NBC kwa ushirikiano wao na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), wa kuandaa mikakati madhubuti ya kuhudumia jamii, hususani waathirika wa ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya Uzazi na aliwasihi waendelee kushirikiana ili kulinda afya za wananchi na kukuza mchezo wa riadha nchini, hasa mbio ndefu. mwandishi wa matukio daima John Mapepele anaripoti kutokea Dodoma

Bashungwa aliyasema hayo Novemba 7, 2021 kwenye hotuba yake akiwa Mgeni Rasmi aliyemwakilisha  Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mbio za NBC Dodoma Marathon 2021 kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

“Dhumuni ya mbio hizi, ni kuchangia vita dhidi ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi. Ugonjwa huu ndio unaoongoza kwa vifo vinavyosababishwa na saratani hapa nchini. Tumesikia kwamba mwaka jana NBC ilichangia jumla ya TZS 100 milioni, fedha zilizotokana na usajili wa wakimbiaji, na michango ya wafadhili mbalimbali”. Aliongeza  Bashungwa.

Aidha, alisema amefurahishwa na uamuzi wa Benki hiyo kuingia mkataba wa miaka mitano na RT, wa kuendesha mbio hizi katika jiji la Dodoma ambapo alisema uamuzi huo utalifanya jiji la Dodoma kuwa na tukio kubwa la mchezo wa riadha, unaovutia washiriki kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

Pia aliupongeza uongozi wa benki ya NBC, na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kwa kuandaa mbio hizo ambapo alieleza kuwa zimeleta hamasa, na mwitikio mkubwa wa wananchi, na wakazi wa Jiji la Dodoma.

“Wakazi wa jiji la Dodoma napenda kuwapongeza kwa kushiriki vizuri katika mbio hizi. Hizi mbio zinatarajiwa kuwa mbio kubwa sana katika siku za usoni, na hivyo ushiriki wenu kwa wingi, katika mbio hizi ndio nguzo ya mafanikio. Vilevile ushiriki wenu utachangia vilivyo, katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi. Hii sio kwa Dodoma pekee, bali nchi nzima. Nawasihi wakazi wote hasa vijana na wakinamama, mjitokeze kwa wingi kuliko leo ili sote tuchangie katika mapambano haya”Alifafanua  Bashungwa

Pia kupitia tukio hilo aliwashukuru wafadhili waliofanikisha kufanyika kwa kwa mbio hizo na alisema kuandaa tukio kama hilo, kunahitaji ubunifu mkubwa, moyo wa kujitolea, ushirikiano, na nia njema kwa jamii inayozunguka.

Kwa upande mwingine Bashungwa alisema amefarijika kusikia kwamba Benki imeingia mkataba na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania bara, kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu.

“Ni jambo jema na la kupewa sifa. NBC pia wanaisaidia Taifa Stars, wamedhamini Samia Cup 2021, na NBC ni washirika wa Tanzanite Women Sports Festival. NBC muendelee na sera yenu ya kuwakaribia wananchi kupitia michezo”. Alipongeza  Bashungwa

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI