Chama cha ACT Wazalendo kimelitaka Jeshi la Polisi kuacha kuendelea kumshikilia kituoni mwanamuziki, Vital Maembe.
Taarifa kwa Umma iliyosainiwa na Katibu Idara ya Haki za Binadamu na Makundi Maalum ACT Wazalendo Taifa, Mbarara Maharagande Novemba 3,2021 ilisema kwa siku mbili sasa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea kumshikilia Mwanamuziki Vitali Maembe ambaye mwaka 2020 aligombea Ubunge katika Jimbo la Bagamoyo kwa tiketi ACT Wazalendo.
Maharagande alisema, Maembe ambaye jana Novemba 2, 2021 alishikiliwa na Jeshi la Polisi Bagamoyo kisha baadaye kuhamishiwa Kibaha, alihojiwa na Jeshi hilo kwa tuhuma ya kuwakashifu viongozi kupitia wimbo wake wa Kaizari.
Alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa Jeshi hilo na Serikali kwa ujumla wake kuwazuia wasanii kufanya sanaa zao zenye kuelezea hali halisi ya maisha ya Watanzania kupitia "Nyimbo za Ukombozi"
Mwanasheria wa Chama Bonifasia Mapunda alifika Kibaha pia aliweza kuonana na kuzungumza na Maembe, na pia alionana na Uongozi wa Juu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani juu ya suala hili kwa lengo la kufuatilia na kuhakikisha kuwa Vitali Maembe anaachiwa huru.
"Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kumuachia mara moja Vitali Maembe, na ikumbukwe kuwa ukweli kupitia sanaa hauwezi kuwa Jinai wala uhalifu."alisisitiza Maharagande katika taarifa yake hiyo.
Mkuu wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyegesa hakupatikana mara moja kuzungumzia suala hilo.
0 Comments