Na Frederick Siwale -Mdtv Njombe.
WADAU wa soka katika halmashauri ya Mji Makambako Mkoani Njombe, wameuomba Uongozi wa Klabu ya Mbeya road fc ya Makambako kubadilisha jina ili kuendana na matakwa ya Wadau wa soka katika Halmashauri ya Mji Makambako na Mkoa wa Njombe kwa ujumla wake.
Rai hiyo imetolewa na mdau wa michezo Oscar Mangula katika Halmashauri ya Mji Makambako wakati wa mchezo wa Kirafiki Kati ya Mbeya road fc na timu ya Kijiji cha Kifumbe, Kifumbe fc .
Mangula alisema timu ya Mbeya road fc (Watoto wa nyumbani Makambako) ni timu ya Makambako Kama kauli mbiu yake ilivyo lakini kwa mwananchi wa kawaida anaposikia Mbeya road fc mawazo na fikira zake ni kwamba timu hiyo ni sehemu ya Mbeya city na Mbeya kwanza timu ambazo zote zipo Mkoani Mbeya.
Aidha Mangula alisema timu ya Mbeya road fc inafahamika sana kwani tangu mwaka 1997 ilikuwepo na ilianzishwa na vijana waliokuwa eneo la Mbeya road barabara kuu ya Iringa Mbeya na ndiyo sababu ya kuitwa Mbeya road fc lakini wakati umefika wa kubadili jina ili Wadau wanapoichangia ijulikane ni mali yao.
Katika mchezo huo wa Kirafiki timu ya Kijiji Kifumbe fc iliweza kuibuka washindi kwa mikwaju ya penati 3 - 2 na hiyo ni baada ya kufungana 1-1 hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika.
Timu ya Mbeya road fc ipo ligi daraja la tatu ili hali timu ya Kijiji cha Kifumbe bado inaendelea kucheza mechi za mchangani.





0 Comments