Timu ya Netiboli ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeingia hatua ya robo fainali katika Mashindano ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yanayoendelea mjini Morogoro.
Timu hiyo imefika hatua hiyo baada kuifunga timu ya Netiboli ya Tume ya Waalimu leo Oktoba 25 kwa jumla ya magoli 37:08 huku wakicheza mchezo mzuri wa kuonana vema kwa kufuata maelekezo ya mwalimu wao Alice Choaji ambaye alisema nia yao ni kuchukua ubingwa wa mashindano hayo.
“Timu ipo vizuri na wachezaji wanaendelea kufuata maelekezo vizuri tuliyofundishana wakati wote wa mazoezi, kwa kweli wanatia moyo maana kila tunapofanya mazoezi kujiaandaa na michezo wanaendelea kuwa bora zaidi” alisema mwalimu huyo.
Timu zilizoingia hatua ya robo fainali katika kundi B ni Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi na kuzibwaga nje ya mashindano timu za Tume ya Walimu, Wizara ya Nishati na timu ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA).
Siri kubwa ya ushindi wao ni wachezaji wakati wote kuwa makini kuzingatia na kuzifuata kanuni za mashindano hayo ambapo wachezaji pamoja na viongozi wa timu walifuata barabara ikiwemo kutumia lugha ya kiungwana wakati wote wa mchezo kwani hairuhusiwi kutoa lugha chafu ya matusi au kashfa kwa mwamuzi, kiongozi au mchezaji mwenzake wakati wote wa mashindano hatua iliyowafanya waonane vyema na kutimiza lengo lao kama timu.
Kuimarika kwa timu hiyo na kufanya mazoezi ya wachezaji imewafanya miili kuimarika kimchezo zaidi na kuwafanya wawe katika hali bora zaidi ya kucheza vema katika hatua ya makundi ambapo mchezo unachezwa kwa muda wa dakika 40 kwa michuano ya awali na kuwafanya waweze kuhimili ushindani wa robo fainali ambapo mchezo utachezwa dakika 60.
Pia Mwalimu Alice alisema ushindi wao unachagizwa na ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa Wizara na wachezaji ambapo amewashukuru Viongozi hao wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi ambaye amewakilishwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Bw. Bernard Marcelline ambaye mara zote amekuwa na timu bega kwa bega wakati wote wa mashindano hayo.
Aidha, Mwalimu Alice aliwataka wachezaji hao wasiridhike na matokeo hayo bali wakaze mwendo na kujiandaa ipasavyo na michezo inayofuata ili kupata ushindi zaidi ambao kwao hiyo ni hatua njema na wanadhamiria kuwa na timu ya kudumu ya Wizara itashiriki mashindano mbalimbali yanayosimamiwa Chama cha Mpira wa Netiboli nchini (CHANETA) pamoja na mabonanza mbalimbali.





0 Comments