Header Ads Widget

TAKRIBANI WATU 2000 WAMESHIRIKI MBIO ZA CAPITAL CITY MARATHON

 


Na Doreen Aloyce, Dodoma


Takribani watu elfu mbili (2000) wameshiriki kwenye mbio za  Capital City Marathon zilizofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM huku wakisema imekuwa fursa kuijua makao Makuu sambamba na kujenga miili yao kiafya.


Mbio hizo zilizo dhaminiwa na Shirika la Bima la Taifa NIC zimeongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Akosn.


Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa mbio hizo, Dkt Tulia amesema mbio hizo zimeunga mkono adhma ya serikali  ya kuhakikisha inapiga vita magonjwa yasiyo ya kuambikiza .


‘’ Nashukuru kwa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan ambaye anasisitiza wananchi kufanya mazoezi , niwaombe kila mmoja wetu akawe balozi huko tunakotoka, matukio haya yanapokuwepo mahali yanafanya mambo mengi ikiwemo lile la afya kwa sisi tuliofanya mazoezi ’’ amesema



Kwa upande wake , Mkurugenzi wa Masoko na Huduma kwa Wateja Shirika la Bima la Taifa (NIC)  Yessaya Mwakifulefule ,amesema mbio hizo ni mbio ambazo hupanda thamani kila mwaka hivyo husaidia kwa kiasi kikubwa kutengeneza ajira kwa vijana .



‘’NIC tumedhamini mbio hizi kupitia bidhaa yetu ya Bima ya Makazi  tukiwataka watanzania waweze kulinda makazi yao , hii si mara ya kwanza kwa NIC kushiriki kwenye michezo mbalimbali kwa maana ya riadha, mpira wa miguu, kwasababu tunaamini michezo ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana na hata serikali yetu inasisitiza kwamba vijana wajiajiri kupitia michezo’’ amesema



Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Michezo Nsolo Mlozi, amepongeza jitihada zinazofanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  katika kufanikisha mazoezi kwani imeweza kurahisisha maisha ya watanzania.


Nsolo Mlozi amesema wameona ni bora kuendeleza adhma ya  mbio hizo ili kudumisha michezo pamoja na kujenga afya ambapo pia wanatumia fursa hiyo kutangaza vivutio vilivyopo makao Makuu ya nchi kutokana na Wengi kusikia kupitia vyombo vya Habari.



‘’Jiji la Dodoma limepata wageni wengi waliohamia ,muda unapatikana mwingi sana jioni tunapotoka ofisini, kwahiyo tukaona tuboreshe urafiki wetu na undugu wetu katika michezo ,sambamba na hayo tumekuwa tukifanya shughuli mbalimbali ikiwemo mbio za michezo kwa kila mwezi"amesema Mlozi


Ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kujitokeza kwenye mashindano hayo ambayo yanasaidia kuepukana na magonjwa ambayo yanaweza kuwashambulia sambamba na kudumisha urafiki.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI