Waziri wa nishati ,January Makamba
Na Kilanga, MDTV Arusha
Serikali kupitia shirika la mafuta Tanzania(TPDC) imeanza kununua shehena ya mafuta moja kwa moja ya dizeli kutoka kwa wazalishaji wa nchi rafiki zanazozalisha mafuta ili kuondokana na changamoto ya gharama kubwa kwa wanunuzi wa kati.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyikia jijini Arusha,Waziri wa nishati ,January Makamba alisema kwa mara ya kwanza ile azma ya miaka mingi ya serikali kununua shehena ya mafuta moja kwa moja kutoka kwa wazlishaji sasa imetimia.
"Hata kabla ya mwisho wa safari yetu mnamo,Octoba 28 Mwaka huu tuliiwezesha TPDC kushiriki zabuni ya kiushindani na makampuni mengine ya kimataifa ambayo kila mwezi hushiriki zabuni kuleta mafuta nchini,"alisema Waziri Makamba.
Aidha Makamba alisema kuwa TPDC imefanikiwa kushinda zabuni hiyo kwa kutoa bei ndogo zaidi ya kuagiza mafuta ya dizeli kwa Disemba mwaka huu ikiwa hali hiyo itapunguza makali ya bei ya mafuta na kudhihirisha kwamba hatua hiyo ina manufaa.
Waziri Makamba alisema serikali imefanikiwa kushawishi nchi rafiki walizotembelea katika kushirikiana na nchi ya Tanzania kujenga kituo kikubwa cha upokeaji na uhifadhi wa mafuta kwa ajili ya soko la ndani lakini kwa mahitaji ya nchi ya Afrika mashariki na kati na nyingine za mbali pale zinapohitajika.
"Kituo hiki kitatuhakikishia kuwa na kiasi cha kutosha cha mafuta ya ndani ya nchi wakati wote lakini kwa sasa iwapo itatokea dharura huko duniani na tukashindwa kuagiza mafuta kiasi yaliyopo nchini yanatutosheleza kiasi cha wastani wa siku 15 tu,"alisema.
Alisema baada ya wiki mbili kuanzia sasa kutakuwa na ziara ya viongozi na wataalam kutoka katika nchi tulizozitembelea kuja Tanzania kwa ajili ya kukamilisha taratibu za utekelezaji wa makubaliano yao kwenye maeneo waliokubaliana kushirikiana hivyo wizara ya nishati itaendelea kuratibu na kufuatilia ili kuhakikisha kwamba mafanikio yaliyopatikana kwenye ziara hiyo yanadumu na yanatekelezwa kwa maslahi mapana ya nchi ya Tanzania.
Wakati huohuo Makamba alisema katika kuendelea kurekebisha sekta ndogo ya mafuta serikali itaendelea kuhimarisha TPDC kwa kuiruhusu haraka kuajiri watumishi weledi na wajuzi wa biashara ya mafuta ili iendelee kununua mafuta kwa niaba ya serikali kwa ufanisi zaidi
Aidha alisema kwa hatua ya muda wa kati lakini yenye jawabu la muda mrefu serikali itaanzisha hifadhi ya kimkakati ya mafuta ili kuwa na akiba kubwa ya mafuta wakati wotebkwa ajili ya dharura na pale bei duniani itakapopanda kwa kiwango kikubwa na katika kwa kuzingatia mfumo wa uagizaji wa pamoja utasaidia kubaini mapungufu na kuboresha kwa maslahi mapana ya Taifa.
"Kufanya tathmini ya utendaji na watumishi wa taasisi zote za serikali zinazohusika na biashara ya mafuta wa pamoja ili kuhakikisha kwamba taasisi hizi na watumishi wake wote wanatimiza wajibu wao kwa weledi na uadilifu na kwa maslahi ya nchi pamoja na kuendelea na utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo kuendelea kupitia tozo na kodi mbalimbali zinazochangia kuongezeka kwa bei ya mafuta nchini,"alisema Waziri huyo.
Aliongeza kuwa katika kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa biashara ya mafuta nchini ikiwemo TAOMAC na TAPSOA na kuweka mazingira mazuri ya biashara ya mafuta nchini kwa sekta binafsi kuendelea kushiriki ili kuwe na ushindanibwa haki na uwazi kwa manufaa ya watuamiaji mafuta na nchi kwa ujumla pamoja na kuongeza ufuatiliaji wa karibu zaidi kwenye sekta hiyo kwa kutumia vyombo na mamlaka mbalimbali ili kubaini na kudhibiti hujuma na udanganyifu katika biashara hiyo.
Pia alisema katika kurekebisha miundombinu ya upokeaji na uhifadhi wa mafuta nchini hasa kwenye bandari ili kuhakikisha kuna uwepo wa ufanisi zaidi pamoja na kuendelea kuyafanyia kazi na kutekeleza mapendekezo ya tume iliyoundwa na Mheshimiwa Waziri mkuu kuhusu biashara ya mafuta nchini.
Hata hivyo bei ya mafuta nchini kwa kiasi kikubwa inachangiwa na bei za mafuta duniani ambazo serikali ina nafasi ndogi kwenye kudhibiti na serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba yale yaliyo ndani ya uwezo wa serikali katika kudhibiti bei ya mafuta tunayoifanyia kazi.
0 Comments