Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amewasili nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu, ambapo pamoja na mambo mengine atazungumza na mweyejii wake, Rais Samia Suluhu.
Hii si ziara ya kwanza ya Ndayishimiye nchini Tanzania, mwaka jana mwezi Septemba alifaya ziara ya siku moja kwa mwaliko wa Rais wa wakati huo, hayati John Magufuli, ikiwa ni ziara yake ya pili nchini humo tangu aingie madarakani mwezi Juni, 2020.
Tanzania ni nchi ya kwanza kutembelewa na Rais Ndayishimiye mara baada ya kuingia madarakani akichukua nafasi ya hayati Pierre Nkurunziza.
Ndayishimiye alipokelewa na waziri wa mambo ya kigeni wa Tanzania, Liberata Mulamula katika uwanja wa ndege wa Dodoma tayari kukutana na mwenyeji wake Rais Samia, ambaye mwezi Julai mwaka huu alifanya ziara nchini Burundi.
Katika ziara yake ya kwanza mwezi Septemba 2020, Rais Ndayishimiye alisema katika hotuba yake “Tanzania sio nchi rafiki, lakini ni mzazi kwa Burundi”, kwa msaada wake kwenye uhuru wa Burundi.
Katika ziara ya sasa Rais Ndayishimiye anatarajia kutembelea miradi kadhaa ya maendeleo katika jiji la Dar es Salaam, na atatembelea Zanzibar, kwa mujibu wa taarifa ya wazara ya mambo ya nje ya Tanzania.
0 Comments