NA WILLIUM PAUL, Moshi.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Prof. Patrick Ndakidemi ametembelea kampuni ya kuzalisha Vannila na kuongeza thamani ya Natural Extract Industries (NEI) Ltd iliyopo jimboni mwake na kujionea mambo mbalimbali yanayoendelea katika kampuni hiyo.
Mbali na Vannila, kampuni hiyo inachakata na kuongeza thamani ya mazao mengine kama Cocoa, Kahawa na Machungwa ambayo hulimwa Tanzania.
Prof. Ndakidemi aliipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji wa zaidi ya Bilioni 1.3 hapa Tanzania na kudai kuwa ni mchango mkubwa katika pato la Taifa.
Alisema kuwa, kilimo cha Vanilla ni fursa inayoweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wakulima endapo watashiriki, kwani bei ya zao hilo ni nzuri na soko la uhakika lipo.
Ameongeza kwamba, kampuni hii imejikita kwenye kuongeza thamani ya Vanilla na sii kusafirisha malighafi nje kama inavyofanyika kwenye baadhi ya mazao hapa nchini.
Mbunge huyo alisema kuwa kampuni hiyo imesaidia kuwakomboa wakulima wengi kwa sasa inahusisha wakulima 6000 katika mikoa 8 nchini Tanzania ambapo kati ya hao, 1800 wako mkoani Kilimanjaro na 309 wametoka katika Jimbo la Moshi Vijijini.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo imeajiri jumla ya wafanyakazi 105 wa fani mbalimbali ambapo masoko makubwa kwa bidhaa zao yako nchi za Marekani, Jumuiya ya Ulaya (EU), Uingereza, Japan na Afrika ya Kusini.
Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni hiyo Silas Noah amesema kuwa kwa mwaka mahitaji ya Vannila ni tani laki moja na elfu tano, lakini hivi sasa wameweza kuzalisha tani elfu hamsini tu.
Noah alisema kuwa zao hilo limeonekana kuwa na soko kubwa la nje, hivyo ni jukumu la wananchi kuanza kulima Vanilla katika mashamba yao kwa kuzingatia ushauri wa wataalam wa kilimo na kusisitiza kuwa Vanilla hustawi vizuri kwenye mazingira ya kivuli kama yale yanayochanganya kilimo cha Kahawa, Migomba na miti katika shamba moja.
Mwisho.





0 Comments