Header Ads Widget

MAMA MJAMZITO KUTUMIA VILEVI YATAJWA KUSABABISHA MATATIZO YA AFYA YA AKILI KWA MTOTO

 


Na. WAMJW-Dodoma


DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya akili katika Hospitali ya Taifa ya magonjwa ya Akili Mirembe Dkt. Paul Lawale amewaasa akina mama kuacha matumizi ya vilevi wanapokuwa wajawazito ili kuwanusuru watoto walio tumboni kuzaliwa wakiwa na matatizo ya afya ya akili.


Dkt. Lawale amesema hayo jijini Dodoma wakati akisoma tamko la siku ya maadhimisho ya afya ya akili duniani yanayoadhimishwa Oktoba 10 kila mwaka kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima.


Amesema mama mjamzito anapokunywa pombe anamuweka hatarini mtoto atakayezaliwa kwani inaweza kumsababishia  athari katika  ukuaji wa ubongo kwa mtoto aliye tumboni na hivyo kumsababishia tatizo la afya ya akili pindi atakapozaliwa.


“Tunapoangalia ongezeko la watu wenye matatizo ya afya ya akili, lazima tuangalie tangu mtoto anapokuwa tumboni, wapo akina mama wengi wanatumia vilevi wanapokuwa wajawazito hii ina athari kwa mtoto aliye tumboni”. Amesema Dkt. Lawale.


Ameongeza kuwa Mama mjamzito anapotumia vilevi inasababisha ukuaji wa ubongo wa mtoto kuathirika na kusababisha mtoto kuzaliwa na matatizo ya afya ya akili na kuendelea kuongeza idadi ya wagonjwa wenye matatizo ya afya ya akili nchini. 


Vile vile ametaja sababu nyingine inayosababisha matatizo ya afya ya akili ni pamoja na mtoto kutopata lishe bora tangu anapozaliwa, kufanyiwa ukatili mbalimbali ikiwemo vipigo na manyanyaso mbalimbali. Pia ametaja sababu nyingine za kurithi kutoka kwa wazazi au ukoo.


“Pia kuna wale ambao wana vinasaba vya matatizo hayo katika ukoo, akipata changamoto kidogo tu katika maisha anajikuta anapata matatizo ya afya ya akili lakini umasikini, matatizo kazini yote hayo huchangia mtu kupata matatizo ya afya ya akili”. Amesema Dkt. Lawale.



Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutoka Wizara ya Afya Shedrack Makubi amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha  watanzania milioni saba wana matatizo ya afya ya akili huku akiutaja mkoa wa Dar es salaam  kuwa kinara kwa kuwa na watu wengi wenye matatizo hayo huku akitaja watu zaidi ya milioni 300 wana matatizo ya afya ya akili duniani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI