Header Ads Widget

MAMA AUA WATOTO KWA KUWACHINJA NAYE AFA KWA KUJICHINJA


Na Bahati Sonda, MDTV Maswa.

Ng'washi Makigo(35)mkazi wa kijiji cha Gula wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu amewaua watoto wake wawili kwa kuwachinja na kisha naye kujichinja hadi kufa.


Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa polisi Mkoa wa Simiyu Kamishina Msaidizi wa Polisi,Blasius Chatanda amesema kuwa limetokea Oktoba 22 mwaka huu majira ya saa 2:30 asubuhi katika kitongoji cha Mwatambuka kilichoko katika kijiji cha Lalago wilayani humo ndani ya nyumba ya Luja Makigo ambaye ni mdogo wake na marehemu.


Kamanda Chatanda amewataja watoto hao waliouawa kuwa ni Nseya Kisena(7)ambaye ni  wa kike na Majana Kisena(1.5)ambaye ni wa kiume na kwamba miili ya marehemu hao imekutwa ikiwa ndani ya chumba kimoja.

Chatanda ameeleza kuwa uchunguzi wa awali wa tukio hilo la mauaji umeonyesha kuwa mama huyo alianza kutekeleza mauaji hayo kwa kumchinja hadi kumuua mtoto wake mkubwa ambaye ni Nseya na baadaye kumchinja mtoto wake mdogo ambaye ni Majaba.

Ameongeza kuwa baada ya mama huyo kufanya mauaji hayo ya kinyama naye alijichinja hadi kufa kwani kisu kinachodaiwa kutumika katika mauaji hayo kimekutwa shingoni mwake.

Aidha mwenyeji wa marehemu hao, Luja Makigo ambaye ni mdogo wake na marehemu  Ng'washi Makigo alibaini tukio hilo baada ya kutoka kwenye Zahanati ya kijij cha Gula ambapo alikwenda kwa ajili ya matibabu.

Kamanda Chatanda ametaja chanzo cha tukio hilo ni ugonjwa wa akili kwani mdogo wa marehemu ameeleza kuwa dada yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili na siku za nyuma aliwahi kufanya jaribio la kujiua kwa kujikata na wembe sehemu za shingoni lakini hakufanikiwa.

Hata hivyo jeshi la polisi mkoa wa Simiyu linatoa wito kwa wananchi kuongeza umakini kwa watu wanaosumbuliwa na matatizo ya ugonjwa wa akili ili wasiweze kuleta madhara kwa jamii.

            

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI