Na Mapuli Misalaba,MDTV Shinyanga
Madiwani wa Kata mbalimbali za Manispaa ya Shinyanga wamekemea tabia ya mkandarasi mmoja kupewa zabuni zaidi ya moja hali inayopelekea kucheleweshwa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleleo.
Wakizunguma katika kikao cha baraza la madiwani viongozi hao wamesema kuwa hali ya wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA mkoa wa Shinyanga kupewa zabuni katika kata Tano za Manispaa ya Shinyanga inakwamisha ukamilishaji wa barabaraba kwa wakati.
Wameongeza kuwa kuna baadhi ya wakandarasi waliopewa zabuni na TARURA mkoa wa Shinyanga wanaoishi mkoa wa Dar es salaam wakati ofisi zipo mjini Shinyanga hali inayokwamisha ukamilishwaji wa miradi hiyo.
Aidha madiwani hao wameiomba TARURA kutatua changamoto ya kukosekana kwa mitaro katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ili kupunguza mafuriko kipindi cha mvua kinapoanza.
Akizungumza katika kikao hicho cha baraza la madiwani mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomary Satura amesema machinjio ya kisasa inayojengwa katika eneo la Ndembezi itaanza uzalishaji mwezi Novemba mwaka huu.
Amesema kuwa ujenzi wa machinjio hayo utakuwa umekamilika kwa asilimia mia moja na kwamba itakuwa ni machinjio ya pili yenye kiwango chenye ubora hapa nchini
“Machinjio yetu ya kisasa ya Ndembezi itaaza kufanyakazi inawezekana machinjio yetu yakawa niya pili kwa ubora na tunaamini kwa kufanya hivyo sasa tutakuwa tumeendana na kukidhi matakwa ya jamii yetu ambayo inatamani kuona machinjio ikitoa huduma”
Akizungumzia kuhusu soko la Ndala mkurugenzi huyo ameshauri ujenzi wa soko hilo kuingizwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 badala ya kutumia nguvu kuwalazimisha wafanyabiashara kufanyia shughuli zao kwenye eneo hilo ambalo halina mazingira ya kuvutia
“Tujaribu kupeleka huduma kadri ya mahitaji ya jamii na tusiwalazimishe watu kwa sababu ya mipango yetu miundombinu iliyopo pale kuanzia meza na vibanda vyote havina ubora wa kumshawishi mtu kwenda kufanya biashara vinginevyo tutatumia nguvu kubwa za kupambana na wananchi kuwalazimisha kwenda kufanya biashara kwenye eneo ambalo bado hawana ridhaa nalo”
Mkurugenzi huyo amesema dhamira ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na stahiki za kijamii ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ya barabara, maji na machinjio ya kisasa
0 Comments