Header Ads Widget

KOREA KASKAZINI YARUSHA KOMBORA KATIKA BAHARI INAYOPAKANA NA JAPAN

Korea Kaskazini imerusha kombora angalau moja la balistiki ndani ya maji kwenye pwani ya Japan,  huku wakuu wa ujasusi wa Korea Kusini, Japan na Marekani wameripotiwa kukutana huko Seoul kujadili kuhusu Korea Kaskazini.

Katika wiki za hivi karibuni, Pyongyang imeanza majaribio kadhaa ya kile inachodai kuwa ni makombora ya kusafiri kwa masafa marefu, na silaha za kupambana na ndege ambapo baadhi ya majaribio haya yanakiuka vikwazo vikali vya kimataifa.

Korea Kaskazini imekatazwa haswa na Umoja wa Mataifa kujaribu makombora ya balistiki pamoja na silaha za nyuklia.

Siku ya Jumanne Wakuu wa jeshi la Korea Kusini walisema kombora moja lilizinduliwa kutoka bandari ya Sinpo, mashariki mwa Korea Kaskazini ambapo Pyongyang kawaida huweka manowari zake. Ilitua katika Bahari ya Mashariki, pia inayojulikana kama Bahari ya Japani.

Korea Kaskazini imeendelea mbele na majaribio yake ya makombora kwani Korea Kusini pia inaunda silaha zake, kwa kile waangalizi wanasema kumegeuka kuwa mashindano ya kujikusanyia silaha kwenye peninsula ya Korea.

Hivi karibuni Seoul ilizindua kombora lililozinduliwa na manowari, na inaanda kile kinachosemekana kuwa maonyesho makubwa zaidi ya ulinzi Korea Kusini kuwahi kutokea wiki hii pia inatarajiwa kuzindua roketi yake ya angani hivi karibuni. 

Korea Kaskazini na Kusini zinasalia vitani kwani Vita vya Korea, ambavyo viligawanya peninsula kuwa nchi mbili, vilimalizika mnamo 1953 na mkataba wa kusitisha mapigano lakini sio wa amani .

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un alisema wiki iliyopita kwamba hataki vita vitokee tena kwenye rasi ya Korea, lakini akasema nchi yake inahitaji kuendelea kutengeneza silaha za kujilinda dhidi ya maadui, ambao ni Marekani aliyoishutumu kwa uhasama .

Katika saa 24 zilizopita , mjumbe wa Marekani nchini Korea Kaskazini Sung Kim amesisitiza msimamo wa utawala wa Biden kwamba iko wazi kukutana na Korea Kaskazini bila masharti yoyote.

Mazungumzo ya hapo awali kati ya Amerika na Korea Kaskazini yalivunjika kwa sababu ya kutokubaliana kwa kimsingi juu ya uharibifu wa silaha za nyuklia.

Marekani inataka Korea Kaskazini itoe silaha zake za nyuklia kabla ya vikwazo kulegezwa, lakini Korea Kaskazini hadi sasa imekataa.

Chanzo; BBC Swahili.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI