Uongozi wa shule ya Msingi Kising’a iliyopo Kijiji na Kata ya Kising’a Tarafa ya Isimani wametoa pongezi kwa shirika la EEPICO pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa ufadhili walioupata kupitia shirika la Umoja wa Mataifa UNICEF.
Akitoa pongezi hizo jana wakati wa siku ya unawaji mikono Duniani iliyofanyika kimkoa Katika shule ya Kising'a Mwalimu mkuu wa shule hiyo Ales Mahelela alisema kuwa ujenzi wa miundo mbinu hiyo ulianza Novemba mwaka 2020 kupitia nguvu ya wanakijiji ambao walikusanya mawe , kokoto, mchanga, kushimba shimo pamoja na huduma za maji ambapo Shirika hilo likatoa kiasi cha shilingi Milioni 44,220,000/= za kitanzania kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo, ambapo ujenzi huo umegharimu jumla ya kiasi cha shilingi Milioni 48,440,000/=.
‘’wametujengea vyoo bora vya kisasa vyenye matundu matano kwa ajili ya wasichana, matundu manne kwa wavulana, chumba cha wenye mahitaji maalumu , chumba cha wasichana waliopevuka pamoja na vyoo vya walimu kwani hapo mwanzo havikuwa katika hali ya ubora’’, alisema Bwana Mahelela.
Alisema kuwa shule hiyo imebahatika kupata fedha kutoka Serikali kuu kiasi cha shilingi Milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na ofisi wakishirikiana na wanakijiji waliochangia maji pamoja na madini ujenzi yenye thamani ya shilingi milioni 10,660,000/= pia wanatarajia kuongeza matundu sita ya vyoo kutokana na fedha za mradi wa EP4R ambapo ujenzi huo utaanza hivi karibuni.
Usafi wa mazingira unaendeshwa na club iitwayo SWARSH ambapo unafanyika mara kwa mara huku suala la unawaji mikono kwa wanafunzi popote watakapokuwepo likipewa kipaumbele ili kuweza kujikinga na magonjwa mbalimbali.





0 Comments