Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameungana na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Fredrick Shoo kwenye maombi maalumu ya kuadhimisha miaka 50 ya Hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC), ambapo shughuli hiyo ilifanyika Oktoba 16, 2021 mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Hospitali hiyo ya KCMC ya Kanda ya Kaskazini ambayo inamilikiwa na KKKT, huku ikiwa na ubia na Serikali, ilianzia kwenye Milima ya Usambara mwaka 1926 kwenye Kijiji cha Bumbuli (sasa Makao Makuu ya Halmashauri ya Bumbuli) katika Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga. Lakini kutokana na sababu zisizozuilika, hospitali hiyo ilihamishwa na kupelekwa Moshi mkoani Kilimanjaro mwaka 1971.
Wakati KCMC wanatimiza miaka 50, Hospitali ya Bumbuli ambayo bado inamilikiwa na Kanisa la KKKT kwa ubia na Serikali, ifikapo mwaka 2026 itakuwa inatimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.
Hospitali ya Bumbuli, ndiyo hospitali ya kwanza kuanzisha Chuo cha Tabibu nchini. Ambapo watu mbalimbali walipata utaalamu wa utabibu (udaktari) kutoka hapo, ambapo hadi sasa chuo hicho bado kipo na kinatoa fani ya afya kwenye taaluma mbalimbali.
MKOA WA TANGA: Tanga tuna mengi ya kujivunia ikiwa pia ni watu wa kwanza KUWA WASTAARABU (KUPATA ELIMU). Elimu iliingia kwenye nchi ya Tanganyika (sasa Tanzania) kupitia Mkoa wa Tanga, ikitokea Zanzibar. Ambapo shule za kwanza za msingi na sekondari zilianzia wilaya ya Muheza, ambapo mwaka 1858 Shule ya Sekondari ya Kwanza ilijengwa eneo la Magila- Msalabani chini ya Wamisionari wa Kanisa Anglikana. Na shule ya sekondari ya kwanza ya Serikali ilijengwa mjini Tanga mwaka 1895 (Tanga School). Baadae shule za msingi zilienea Lushoto, Korogwe, Handeni na Tanga. Hata chuo cha kwanza cha ualimu kilianzia Kiwanda, Muheza kwenye Kata ya Tongwe, na baadae kuhamishiwa Korogwe (sasa Chuo cha Ualimu, Korogwe- TTC) mwaka 1965.
Ikulu ya Magamba, Lushoto ilianza kabla ya Magogoni, Dar es Salaam. Na pia Ikulu hiyo, yalikuwa Makao Makuu ya Magavana wa Kikoloni wa Ujerumani na Uingereza kwa nchi za Afrika Mashariki, ambapo walikuwa wanakaa Lushoto, lakini shughuli zao wanafanya Tanzania, Kenya na Uganda. Hata Magavana wa mwisho wa Uingereza Edward Twinning na Richard Turnbull walikuwa wanaishi hapo.
Na Wajerumani walikuwa wanajenga reli kwenda Lushoto, na kama sio Vita ya Kwanza ya Dunia 1914-1918, kungekuwa na treni kutoka Lushoto hadi Mombo, na baadae kuunganika na ile ya Dar es Salaam- Moshi- Arusha. Kwani reli hiyo ilikuwa inajengwa, na ilifikia maeneo ya Madala, Kata ya Ngulwi, Lushoto, lakini mwaka 1919, Wajerumani walikimbia kutokana na vita, na kuachana na ujenzi huo.
Hata Makao Makuu ya Jeshi la Polisi yalikuwa wilayani Lushoto. Pia Lushoto ilikuwa na namba zake za magari zikifahamika kama US yaani Usambara. Pia ilikuwa na fedha yake, na Utawala wake wa Kichifu chini ya Chifu Kimweri, ambaye alitawala kwenye maeneo ya baadhi ya Mkoa wa Tanga (ikiwemo maeneo ya Wilaya ya Same), ambapo kabla ya Uhuru mwaka 1961, Wilaya ya Same ilikuwa sehemu ya Mkoa wa Tanga.
Hata Msomi Mbobezi (wakati huo) ambaye alichangia maendeleo ya Tanga, John Keto (ambaye alizaliwa mwaka 1918), huku baba yake mzazi mzee Vuo ambaye ni Msambaa aliyetokea maeneo ya Mlalo, Lushoto na kwenda kuwa Padre wa Kanisa Anglikana Magila- Msalabani, wakati anakuwa Mbunge wa Jimbo la Tanga mwaka 1958 wakati wa KURA TATU, jimbo lake la Tanga lilikuwa hadi Same, huku Mbunge wa Morogoro (mwaka huo 1958) Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alikuwa ni SWAHIBA mkubwa wa John Keto wakisoma wote Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda na baadae Chuo Kikuu cha Edinburgh, Scotland ambako wote walipata Masters, Jimbo lake la Morogoro alikuwa anakwenda hadi Mzizima (Mkoa wa Dar es Salaam).
Dola ya Wasambaa chini ya Chifu Kimweri, pia ilikwenda hadi maeneo ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ilivuka hadi Zanzibar, ambapo Ikulu ya Zanzibar ipo eneo la Vuga, sababu Chifu Kimweri alianza kukaa yeye eneo hilo, na jina hilo alitoka nalo Vuga ya Lushoto ambako ndipo yalipokuwa Makao Makuu yake ya UTAWALA (yaani KITALA kwa Kisambaa), ambayo sasa ni Kata ya Vuga, Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto. Pia utawala wake ulivuka hadi sehemu ya nchi ya Comoro ambapo ndiyo ASILI ya Chifu Kimweri.
Hata Kiwanda cha Uchapishaji cha kwanza nchini ni Vuga Press. Kiwanda hicho ambacho kinamilikiwa na Kanisa la KKKT, kilianzishwa mwaka 1912. Na kwa sasa kipo mjini Soni pembezoni mwa barabara ya Soni- Mombo. Kwa wale waliosoma miaka ya 1950, 1960, 1970 na kidogo 1980, watakumbuka vitabu vingi vikiandikwa na akina Raphael Shempemba, ambaye kwa wakati fulani alikuwa Mbunge wa Jimbo la Lushoto, vilikuwa vinachapwa Vuga Press.
Hayo ni kwa uchache, lakini Tanga ndiyo ilikuwa Tanzania. Hata mradi wa kwanza wa umeme wa kutumia maji ulianza Tanga kwa kujengwa Hale, Korogwe mwaka 1934. ambapo walishirikiana na Dar es Salaam nao wakapata umeme huo. Tanga ndiyo mkoa wa kwanza kuwa na barabara za lami. Na Wazungu waliweka lami kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Lami hiyo ilianzia Bandari ya Tanga hadi Kijiji cha Mkumbara, Kata ya Mkumbara, Tarafa ya Mombo, Wilaya ya Korogwe yenye urefu wa takribani kilomita 170 kwenye barabara kuu ya Dar es Arusha, ambapo hapo ilikuwa ndiyo mwisho wa mashamba ya mkonge ya Mkoa wa Tanga, sababu walilenga viwanda vyote vilivyopo pembezoni mwa barabara hiyo zaidi ya 50, mazao yao ya mkonge yasafirishwe kwa uhakika ili kufika kwenye viwanda mjini Tanga, na kusafirisha nje ya nchi.
Lakini kwa kuwa na mashamba ya mkonge, ilifanya Tanga kuwa Kitovu cha Uchumi Duniani. Kuna watu waliokuja kuwekeza kampuni, mashirika, viwanda na shughuli mbalimbali za kiuchumi. Pia kuna watu walitembea kwa miguu kutoka mkoani Ruvuma zaidi ya kilomita 1,100 kuja Tanga kutafuta kazi ya vibarua. Na wilayani Korogwe (Old Korogwe), ndiyo kulijengwa kambi ya kupokea wafanyakazi wa kuhudumu mashamba ya mkonge SILABU (Sisal Labour Bureau) maarufu kama MANAMBA. Wafanyakazi wengine walitoka nchi za Msumbiji, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Congo ya DRC, Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya.
Kuna mengi ya kujivunia Tanga. Tanga ya Kijani. Tanga ya Bahari, Mito na Maziwa. Tanga ya misitu minene yenye miti yenye umri wa miaka zaidi ya 500 kwenye Tao la Mashariki ambalo linapita kwenye wilaya nne za Mkoa wa Tanga yaani Mkinga, Muheza, Korogwe na Lushoto, maeneo ya Amani, Muheza, Maramba, Mkinga, Magoma na Bungu, Korogwe na Mazumbai, Magamba na Mbaramo, Lushoto. Hivyo Tanga ina vigezo vyote kuwa mikoa miwili, ambapo mkoa mmoja utabeba jina la Tanga, na mwingine utaitwa Mkoa wa Usambara.
Usambara ina maana kubwa kuliko kitu chochote kwenye ukanda huu, kwani jina hilo limebeba mambo mengi. Mkoa wa Tanga kwa sasa ndiyo wenye kata nyingi 245, wilaya nyingi (8), halmashauri nyingi (11), wabunge wengi (15), ambapo 12 wa majimbo na watatu Viti Maalumu. Na ili maendeleo ya wananchi yafikiwe kwa haraka ni kupunguza mgawanyo ya maeneo ya utawala. Ambapo mafungu yaliyokuwa yanakwenda kwenye kata moja, mafungu hayo hayo yatakwenda kwenye kata mbili, japo naelewa kuna uwiano wa watu katika kupanga shughuli za maendeleo kwa ukubwa wa eneo na wingi wa watu, lakini eneo la mraba nalo lina umuhimu wake katika kupanga maendeleo.
Na hilo tumelishuhudia wakati wa mgawanyo wa halmashauri mbili za Korogwe, ile Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe (DC), na Halmashauri ya Mji Korogwe (TC). Kumekuwa na kasi ya utengenezaji wa barabara, ujenzi wa shule za msingi na sekondari, masoko, nyumba za walimu, hospitali za wilaya sasa zipo mbili, vituo vya afya, zahanati, na sasa kunakwenda kuwa na Stendi Kuu za Mabasi mbili kwenye Wilaya ya Korogwe.
UMEFIKA WAKATI MAMA SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA TANZANIA, KUUGAWA MKOA WA TANGA IWE MIKOA MIWILI. MKOA WA TANGA (WILAYA ZA MUHEZA, MKINGA, TANGA NA PANGANI), NA MKOA WA USAMBARA (LUSHOTO, KOROGWE, HANDENI NA KILINDI).
NB: CHATO KUWA MKOA VIGEZO VYAKE BADO, LAKINI TANGA VIGEZO VYAKE TAYARI, NA ANDIKO LAKE LIPO TAMISEMI BAADA YA KUPITA KWENYE VIKAO MBALIMBALI IKIWEMO MABARAZA YA MADIWANI, KAMATI YA USHAURI YA WILAYA (DCC), ALAT MKOA TANGA NA KAMATI YA USHAURI MKOA (RCC).
Wakatabahu: Yusuph Mussa, Korogwe- Tanga
0 Comments