CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU TUKIO LA OFISI ZA CHAMA WILAYA YA TUNDUMA KUUNGUA MOTO.
Usiku wa kuamkia leo tarehe 13 Octoba,2021 tumepokea taarifa za Ofisi za Chama Wilaya ya Tunduma kuunguzwa Moto ,tukio ambalo mpaka sasa chanzo cha Moto huo hakijajulikana .
Taarifa za tukio hilo zimeshafikishwa katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Tunduma na Polisi wameahidi kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo.
Itakumbukwa kuwa ni mwezi Julai,2021 vijiwe na vizimba vya Chadema katika mji wa Tunduma vilivunjwa na Polisi badala ya kufanya uchunguzi waliamua kuwakamata wanachama wa Chadema na kuwafungulia mashitaka,japo walifuta mashitaka hayo kutokana na kukosekana ushahidi juu ya waliokamatwa kuwa wahusika ! Jambo la kushangaza pamoja na mashitaka kufutwa Ila bado wametakiwa kuwa wanaripoti Polisi kila Juma mara moja .
Aidha, katika Wilaya ya Tunduma wapo viongozi na wanachama wetu 43 ambao wapo katika gereza la Mbozi Kwa tuhuma za kubambikiwa za Mauaji, Unyanganyi wa silaha na Uhujumu uchumi, wapo katika gereza Hilo kwa zaidi ya miezi 12 na kesi Haijaanza kusikilizwa Kwa sababu Polisi wanasema upelelezi haujakamilika . Ikumbukwe Kati ya watuhumiwa hao yupo mama mmoja ambaye alikamatwa akiwa nyumbani kwake na ni mgonjwa wa saratani ya ziwa, anaendelea kuteseka katika gereza hilo bila kupatiwa huduma stahiki za matibabu.
Tunalaani vikali matukio haya ambayo yanaendelea kutokea katika Wilaya ya Tunduma , tunaamini yote haya yanafanyika ili kuwatisha na kuwakatisha tamaa viongozi na wanachama wetu ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kupigania Haki na Demokrasia ya kweli.
Tunataka hatua stahiki na za haraka zichukuliwe ili kuinusuru Amani ya Wilaya ya Tunduma na Tanzania Kwa ujumla ; Hatua hizo ni pamoja na zifuatazo;
1. Jeshi la Polisi Makao Makuu waunde kikosi KAZI Maalum Kwa ajili ya kuchunguza matukio haya ambayo sasa yameshika mizizi katika Wilaya ya Tunduma na watoe taarifa ya uchunguzi wao Kwa UMMA .
2. Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP) atumie mamlaka yake Kwa mujibu wa sheria kuwafutia mashitaka waliyobambikizwa viongozi na wanachama wetu 43 ambao wapo katika gereza la Mbozi Kwa zaidi ya miezi 12 na upelelezi haujakamilika.
3. Vyama vya Siasa na wanachama wao wanaojihusisha na matendo ya kuhatarisha Amani ya mji wa Tunduma, wanapaswa kuchukuliwa hatua mara moja kwani kuhatarisha Amani na usalama wa Tunduma ni kuhujumu uchumi wa Taifa na hasa ikizingatiwa kuwa Mji wa Tunduma ni lango Kuu la kibiashara na nchi za SADC.
Tunaendelea kuwasisitiza Watanzania wote bila kujali dini,rangi,makabila na au itikadi za vyama vyao ,ili Tuendelee kuwa na Amani,utulivu,mshikamano na uchumi imara hatuna budi Kwa Umoja wetu Tuendelee kudai Katiba Mpya ambayo inatokana na maoni ya Wananchi ili tuweze kuwawajibisha viongozi wetu .
Imetolewa Leo Jumatano tarehe 13 Octoba,2021.
John Mrema; Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje





0 Comments