Mahakama kuu ya Tanzania divisheni ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi imetupilia mbali pingamizi lililowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi katika kesi ya msingi nambari 16 ya mwaka 2021 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe pamoja na wenzake watatu.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Kiongozi Mustapha Siyani ambapo amesema baada ya kusikiliza hoja za mawakili na mashahidi watatu watatu kwa kila upande amegundua kuwa ushahidi wa upande wa utetezi hauendani na mapingamizi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika amesema kuwa hawajaridhishwa na maamuzi hayo yaliyotolewa leo na jaji Siyani hivyo wataendelea kuitafuta haki kwa njia nyingine mpaka ipatikane.
''na kama ambavyo hatujaridhika na maamuzi haya bado kisheria na kimahakama ni uamuzi mdogo, ni maamuzi ambayo sisi kisheria tunafungwa mikono ya kuyakatia rufaa, kama kwa mfano hoja hizi zilizoamuliwa na Luvanda na zilizoamuliwa leo na jaji Siyani sheria ingeturuhusu kukata rufaa mapema sana tungepanda mahakama ya juu zaidi ambayo ni mahakama ya rufaa, lakini sheria hairuhusu kwa sasa kukata rufaa hivyo shauri linaendelea baada ya kupangiwa jaji mwingine, tutaendelea kuitafuta hiyo haki kwenye mahakama hii kwa jaji mwingine lakini tutaitafuta hiyo haki kwa njia nyingine ili haki ipatikane kwa wakati'' amesema Mnyika.
Kesi hiyo itaendelea katika ngazi ya kesi ya msingi ambapo iliishia kwa shahidi wa pili wa Jamhuri, ACP Ramadhani Kingai.
0 Comments