Na, Titus Mwombeki-MDTV BUKOBA.
Katika Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba imetengewa kiasi cha Tsh. bilioni 5.57 kwa ajili ya vyumba vya madarasa 208 kwa shule za sekondari Tsh. bilioni 4.16 zimetengwa.
Ikiwawa Vyumba vya madarasa 26 katika vituo shikizi vya shule za msingi 7 vitajengwa vyenye thamani ya Tsh. Milion 520, ujenzi wa bweni kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum imetengwa Tsh. milioni 80, Nyumba za watumishi imetengwa Tsh. milioni 90, majengo ya huduma za dharula imetengwa Tsh. milioni 300 na ununuzi wa mashine za mionzi imetengwa Tsh. milioni 420.
Akizungumza katika kikao cha dharula alichokiitisha Mkuu wa wilaya ya Muleba kwa ajili ya kuanza kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu hiyo Mhe. Toba Nguvila amempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 5.57 na kueleza kuwa fedha hizi zimekuja wakati muafaka ambapo wilaya imeanza mikakati ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa kwa jili ya watoto wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 na kazi ishaanza tayari.
"Nimeona ni vema niwaite viongozi wenzangu ili tuanze kuweka mikakati ya pamoja, kujadiliana namna ya kuweza kuwa na matumizi mazuri ya fedha iliyotolewa na Mheshimiwa Rais ili twende kwa pamoja katika utekelezaji," ameeleza Mhe. Nguvila.
Aidha, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji kukaa na wataalamu wote wa taasisi za Serikali zilizopo wilayani ili kuandaa namna bora ya kutekeleza ujenzi wa miundombinu hiyo hali itakayopelekea kumaliza ujenzi huo kwa wakati.
Sambamba na Hilo, Ngumvila amesisitiza kuanza na madarasa ambayo tayari yalikuwa yameanza kujengwa kwa kukamilisha maboma yaliyopo ili yaweze kuwa tayari kutumika na kubaki na shughuli ya ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu.
Katika mazungumzo yake pia ametoa rai kwa viongozi, wahandisi na wote watakopewa jukumu la kusimamia kwenda kusimamia kwa uadilifu na uaminifu mkubwa kwa kuzingatia ubora wa majengo na thamani ya fedha iliyotolewa ionekane.
"Nisingependa kwa wahandisi kuwa na ufujaji wa fedha kwa kuongeza bei za vifaa na ufundi na kwa viongozi wa Kata, Vijiji, walimu wakuu pamoja na wenyeviti wa vijiji wahakikishe hakuna rasilimali inayopotea ambayo kila kifaa kitakachotolewa wasimamie kwa karibu kitumike kwenye eneo ambalo limepangwa na kwa wakati," amesisitiza Nguvila.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Muleba Ndg. Elias Kayandabila amesisitiza juu ya ushirikishwaji wa jamii kuwa ni vema jamii ishirikishwe kwa kiwango kikubwa hasa kwa kuwatumia viongozi hususani wa Chama Tawala na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kwani wao ndo wana ushawishi mkubwa na namna ya kuwahamasisha wananchi pamoja na kuweka uzalendo katika utekelezaji wa shughuli za umma.
Ameeleza kuwa kwa upande wake atahakikisha anasimamia ipasavyo fedha hizo ikiwemo kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi na gharama za uhenzi wa miundombinu hiyo ili kupata vyumba vingi zaidi ya vilivyokusudiwa huku akisisitiza kufuata maelekezo yanayotolewa ili fedha hizo zitumike kama ilivyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi wa Muleba.Na kuongeza kuwa tayari ameiagiza idara ya ujenzi kuandaa makadirio ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine yenye gharama nafuu.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Muleba Kusini Mhe. Dr Oscar Kikoyo amesema kwa kuwa tayari kuna akiba za benki za matofali katika baadhi ya kata ambayo yamefyatuliwa na kuchomwa na tayari kwa baadhi yao ujenzi wa vyumba vya madarasa umeanza ni vema kuanza kwa kuunga mkono nguvu za wananchi kabla ya kuanza ujenzi mpya. Hivyo basi ujenzi wa maboma unaoendelea ukamilishwe ndio vyumba vingine vipya vianzishwe ikiwemo kuongeza nguvu katika shule mpya zinazoendelea kujengwa kwa nguvu za wananchi.
Naye Mbunge wa jimbo la Muleba Kaskazini Mhe. Charles Mwijage amewasisitiza viongozi kuhakikisha hawawakatishi kasi wananchi waliyonayo ya kujitolea ambapo amesema kuwa wanaweza wasichangishwe elfu kumi za ujenzi wa vyumba vya madarasa badala yake wakashiriki kwenye ujenzi wa madarasa hayo kwa kujitolea nguvu kazi. Pia amesisitiza juu ya kutumia mafundi wanaopatikana katika maeneo ya Kata husika ili kupunguza gharama za ujenzi na sio kutumia wakandarasi.
Na kwa upande Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya, Muleba Magongo Justus amewasisitiza viongozi hususani Wabunge wawe na mpango mzuri wa kuwashirikisha viongozi na wananchi ili kushirikiana na kuhakikisha shule mpya na madarasa mapya yanajengwa.
Kwa upande wake Mdhibiti ubora wa Shule Mwl. Josephat Masiko Joseph ametoa angalizo kwa wahandisi kuhakikisha wanapojenga vyumba vya madarasa wazingatie miundombinu rafiki kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji maalum.
Baada ya kikao hicho viongozi kwa pamoja waliona ni vema kuwa na kikao kingine kilichowajumuisha Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa Kata, Waratibu Elimu Kata na baadhi ya walimu wakuu na wakuu wa shule ambao wameonesha kufanya vizuri katika matumizi ya fedha kwa kujenga kwa gharama ndogo ili kuwashirikisha na wengine waweze kuiga kutoka kwao.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba na kuhudhuriwa na Viongozi wa chama cha Mapinduzi, kamati ya Usalama ya wilaya, Waheshimiwa Wabunge wa jimbo la Muleba Kusini na Muleba Kaskazini, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji, Wakuu wa Idara na wakuu wa Taasisi za Serikali zilizopo wilayani Muleba.





0 Comments