Na Namnyak Kivuyo, Arusha
Baraza la madiwani halmashauri ya Arusha imekataa taarifa ya mradi wa umeme vijijini (REA) kutokana na madai ya kuwa taarifa hiyo haina uhalisia na kinachoendelea katika kata zao kwani kero ya umeme bado haijapata ufumbuzi.
wakiongea kwa nyakati tofauti katika baraza hilo madiwani hao wamesema kuwa wamekuwa wakipewa taarifa ya REA hiyo hiyo kwa miaka mitatu mfululizo huku wakiambiwa kuwa mkandarasi yupo kazini jambo ambalo sio kweli kwani hakuna jambo lolote linaloendelea katika kata zao juu ya suala la umeme.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ojung'u Salekwa ambaye pia Diwani wa kata ya Laroi alisema kuwa kuwa wamekuwa wakisomewa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa REA katika vijiji vyao lakini yaliyopo katika taarifa hizo ni tofauti na kinachoendelea huko kwani hakuna utekelezaji unaofanyika katika maeneo husika yanayotajwa katika taarifa hiyo.
“Hii taarifa sio ya kweli hayo mliyoyaandika huko hayapo huko vijijini anatokea mkandarasi analaza nguzo anafungua transformer anaondoka haonekani zaidi ya mwaka lakini mkija huku mnatuamnia mkandarasi yupo site hii sio kweli,” Alisema Ojung'u
Diwani wa kata ya Musa Elibariki Memboroo alisema kuwa ni muda mrefu umepita tangu Tanesco waonekane kwenye kata huku mashimo waliyochimba kwaajili ya kusimika nguzo yakileta athari kwa mifugo kwani Ng'ombe wamekuwa wakitumbukia katika mashimo hayo wakati wa malisho na kuvunjika miguu.
“Sisi tupo katika kata zetu kila siku tunaona na tunajua kinachoendelea, wananchi wamekuwa wakituuliza juu ya mradi huu lakini hatuna majibu ya kuwajibu leo unakuja na taarifa za mkandarasi kuwepo kazini mbona hatumuoni na madiwani wengine wamesema hapa mnatokea siku moja wananchi wanapata matumaini alafu mkiondoka hamrudi tena kazi inasimama,”Alisema.
Taarifa hiyo iliyosomwa na super survey kutoka Tanesco mkoa Arusha Sydney Mark ambapo alisema kuwa mradi huo unaendelea kutekelezwa katika kata tano za halmashauri hiyo kwa hatua za usimikaji nguzo na ufungaji wa trasnfoma na kuwa mkandarasi yupo kazini kuendelea kuunganishia wananchi umeme.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Arumeru Injinia Richard Ruyango alisema kuwa ameongea na meneja wa Tanesco mkoa wa Arusha na kumpa taarifa za kumtaka kuhudhuria kikao cha DCC kinachotarajiwa kufanyika siku jumatatu ili kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo kwani taarifa hiyo haina ukweli kutokana na taarifa ambazo walizopewa awali juu ya vijiji vilivyoingia kwenye mradi huo kwa awamu ya tatu.
“RAS tukitoka hapa muandikie barua jumatatu aje yeye mwenyewe kwenye kikao asijekusema hakunielewa, waheshimiwa madiwani maswali yenu yote atajibu yeye kama mwenyekiti wabaraza mwenyewe hana umeme nyumbani kwake, madiwani hawana kijiji kizima, shule, Zahanati hakuna umeme tunataka taarifa tangu mkandarasi huyo ameanza kazi amehudumia kata ngapi,” Alisema Injinia Ruyangu.
Alifafanua kuwa watainuka na kwenda maeneo ambayo yanatajwa ili wakaone kero iliyopo na majibu yapatikane kwani serikali ya awamu ya sita haipo katika maneno bali vitendo na majibu yasipo patikana waende kwa waziri mwenye dhamana kwasababu changamoto ya kupewa taarifa isiyo sahihi imekuwa imekuwa ikijirudia mara kwa mara huku watoa tarifa wakiwa wanabadilika.
“Siku zinaenda malalamiko ni yale yale, yeye atoke kwenye mkoa aelekeze macho kwenye halmashauri ya Arusha tunataka aje kutoa majibu na huo ndio utakuwa mzizi wa fitina kwani hali hii inatengenezea serikali mazingira magumu hata mimi nimedanganywa kupitia taarifa hii tunataka kujua mkandarasi huyo kwa fezi hii ya pili amehudumia kata ngapi kati ya kata zetu 27,”Alisema.
0 Comments