NA MATUKIO DAIMA MEDIA
MAFINGA.
Halmashauri ya Mji Mafinga imekanusha taarifa iliyotolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Mafinga, Dkt. Victor Msafiri, kuhusu madai ya kufukuzwa kazi kwa madaktari saba waliokuwa wakihudumu katika hospitali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa mafinga Peter ngussa alieleza kuwa taarifa hiyo ilitolewa katika mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini,Dickson Nathan Lutevele ‘Villa’, uliofanyika Agosti 24, 2026, wakati wa kusikiliza kero za wananchi na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mafinga.
Katika mkutano huo, ilidaiwa kuwa madaktari saba waliokuwa wakifanya kazi katika Hospitali ya Mji Mafinga wamefukuzwa kazi, huku baadhi yao wakielezwa kupangiwa majukumu ya kufanya kazi kwenye gari la Halmashauri linalotumika kubeba taka.
Aidha, katika taarifa hiyo ilidaiwa kuwa kuna madaktari wengine ambao mchakato wa kinidhamu dhidi yao unaendelea kutokana na tuhuma mbalimbali za kiutumishi.
“Hakuna daktari yeyote aliyefukuzwa kazi na kwamba madaktari wote waliopo katika Halmashauri hii wanaendelea na ajira zao na majukumu yao kama kawaida,Halmashauri pia imekanusha taarifa kwamba kuna watumishi walioondolewa kwenye majukumu ya kada zao na kupewa majukumu mengine, ikiwemo kufanya kazi ya ukusanyaji au usafirishaji wa taka kwa kutumia magari ya Halmashauri”alisema
Aidha, Ngusa amesema hakuna mchakato wowote wa kinidhamu unaoendelea dhidi ya wataalamu wa afya, hivyo taarifa zilizotolewa kuhusu suala hilo hazina ukweli kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa na mamlaka hiyo.
Kutokana na taarifa hizo zinazodaiwa kupotosha na kusababisha taharuki miongoni mwa wananchi, Halmashauri ya Mji Mafinga imeomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza, huku ikieleza kuwa itachukua hatua kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma.
TAZAMA VIDEO YA KAIMU MKURUGENZI BOFYA HAPA
Halmashauri imesisitiza kuwa pale inapobainika mtumishi ana tuhuma au amefanya kosa la kiutumishi, hatua za kinidhamu huchukuliwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma, na kwamba hatua hizo hazipaswi kutafsiriwa au kuwasilishwa kwa umma kwa namna inayoweza kusababisha upotoshaji na taharuki.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Mafinga Reginant Kivinge akizungumzia taarifa hiyo katika Mkutano maalumu wa baraza la madiwani wa kujadili rasimu ya taarifa za hesabu za halmashauri ya mji wa mafinga kwa mwaka wa fedha unaoishia june 30,2026.
Amesema taarifa zinazoeleza kuwa Halmashauri ya Mafinga imewafukuza baadhi ya watumishi si za kweli na hazipaswi kuchukuliwa kama taarifa rasmi kutoka kwenye mamlaka husika.
Aidha, amezitaka vyombo vya habari na wananchi kutopotoshwa na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hali ya watumishi katika halmashauri hiyo.
“Kwa niaba ya Baraza la Madiwani na kwa niaba ya Halmashauri, kama Mwenyekiti wa Halmashauri nakanusha taarifa hiyo, Hatujafukuza watumishi na hakuna watumishi walioondolewa kwa suala lolote la utovu wa nidhamu,” amesema.
Ameongeza kuwa watumishi waliopo katika idara mbalimbali wanaendelea na majukumu yao kama kawaida na wamekuwa wakitekeleza kazi zao kwa weledi.
"Changamoto zinazojitokeza katika utendaji zimekuwa zikishughulikiwa kwa njia ya mazungumzo kati ya watumishi, viongozi wa halmashauri na Baraza la Madiwani,licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika utendaji, viongozi, madiwani na watumishi wamekuwa wakishirikiana katika kuzitatua na kujengana kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora”alisema
Mwenyekiti amesema Halmashauri ya Mafinga inaendelea kufanya kazi kwa utulivu na ushirikiano, huku watumishi katika idara mbalimbali wakiendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa lengo kubwa la halmashauri ni kuhakikisha Mafinga inafikia maendeleo yanayotarajiwa na wananchi, hususan katika utoaji wa huduma kwa jamii.VIDEO YA MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA MJI MAFINGA BOFYA HAPA
Aidha, amezitaka vyombo vya habari na wananchi kutopotoshwa na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hali ya watumishi katika halmashauri hiyo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi George Kavenuke amewataka Madiwani kuendelea kushirikiana na wakuu wa Idara pamoja na wataalamu wa halimashauri hiyo ili kuendelea kutekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi.
“ushirikiano wa chama na serikali ni mzuri katika Halmashauri ya Mufindi kuhakikisha miradi inafanikiwa kwa manufaa ya wananchi,hasa katika utendaji wa fedha nampongeza mhasiku amewasirisha taarifa vizuri kuhusu hali ya kifedha, madeni na mapato na matumizi”alisema Kavunike
TAZAMA BARAZA ZIMA LA MADIWANI BOFYA LINK HII
MWISHO.











0 Comments