WAKILI PAUL KISABO ANAKUJA NA JIBU HILI KUWA HAPANA
Ibara ya 47(4)(c) ya Katiba inaweka uanachama na udhamini wa chama cha siasa kama moja ya sifa za mtu kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais. Aidha, Ibara ya 47(4)(d) inamtaka mtu huyo kuwa na sifa zinazomwezesha kuwa Mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Hivyo, kuwa mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa ni sharti la kikatiba katika uteuzi wa Makamu wa Rais.
Hata hivyo, baada ya mtu kushika nafasi hiyo, mazingira ya kukoma kuwa Makamu wa Rais yanaainishwa na Ibara ya 50(2) ya Katiba. Kwa mazingira ya Dkt. Emmanuel Nchimbi, Ibara ya 50(2)(c) inaeleza kuwa Makamu wa Rais ataendelea kushika kiti chake hadi atakapojiuzulu, huku Ibara ya 50(2)(h) ikitambua kukoma kushika nafasi hiyo vinginevyo kwa mujibu wa masharti ya Katiba.
Muhimu zaidi, Ibara ya 50(2) haisemi kwamba Makamu wa Rais anakoma kushika nafasi yake moja kwa moja anapopoteza uanachama wa chama kilichomdhamini.
Hii ni tofauti na nafasi ya Mbunge. Ibara ya 71(1)(e) ya Katiba inaeleza wazi kwamba Mbunge ataacha kuwa Mbunge iwapo ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwa mwanachama wake wakati alipochaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge.
Kwa hiyo, pale Katiba ilipotaka kupoteza uanachama wa chama kusababishe kupoteza nafasi ya kikatiba, imeeleza hivyo wazi. Masharti kama hayo hayajawekwa katika Ibara ya 50 kuhusu Makamu wa Rais.
Dkt. Nchimbi aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu tarehe 25 Agosti 2026 na kubainisha kwamba kujiuzulu kwake kutaanza kutumika tarehe 4 Septemba 2026.
Ibara ya 149(2) ya Katiba inaweka msingi muhimu kuhusu muda wa kuanza kutumika kwa kujiuzulu: pale mtu anapowasilisha kujiuzulu kwake kwa maandishi na kutaja tarehe ambayo kujiuzulu huko kutaanza kutumika, kujiuzulu huko kunakuwa na athari kuanzia tarehe aliyobainisha.
Kwa hiyo, kwa tafsiri ya masharti haya ya Katiba, kufutwa kwa uanachama wa CCM pekee hakumalizi moja kwa moja nafasi ya Dkt. Nchimbi kama Makamu wa Rais. Kwa kuwa katika barua yake alibainisha tarehe 4 Septemba 2026 kuwa ndiyo tarehe ya kuanza kutumika kwa kujiuzulu kwake, basi kujiuzulu huko kunaanza kuwa na athari za kikatiba tarehe hiyo.
Paul Kisabo
Wakili






0 Comments