Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Stephen Wasira ametaka elimu ya katiba ya chama hicho ifundishwe kwa viongozi na wanachama wote nchini ili waweze kusimamia utekelezaji wake lakini kuitetea bila kuogopa.
Wasira alitoa maagizo hayo akizungumza na viongozi na watendaji wa CCM wa ngazi ya wilaya hadi ngazi ya shina wa wilaya Buhigwe na wilaya ya Kasulu akiwa kwenye ziara ya siku moja ya kichama kwenye wilaya hizo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu mkoani Kigoma.
Katika hilo Wasira amemuagiza Katibu wa uenezi,siasa na mafunzo CCM mkoa Kigoma, Deogratius Nsokolo kusimamia maagizo na maeleekezo yake kuhakikisha Makatibu wa siasa, uenezi na mafunzo kwa ngazi za wilaya na kata wanapeleka mafunzo hayo kwa viongozi na wanachama wa ngazi zote hadi matawi akieleza kuwa maagizo hayo yapaswa kutekelezwa nchi nzima
Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM Bara alisema kuwa kwa wanachama wa CCM kwa ngazi zote zikiwemo ngazi za matawi kuijua kwa undani katiba ya CCM kunawapa wigo mpana wa kuisemea na kuitetea bila woga lakini pia kuwa na uwezo wa kujibu hoja na propaganda zinazotolewa na wapinzani.
Aidha katika mkutano huo Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM Bara amesema kuwa miaka 50 ya kuzaliwa CCM mwaka 2027 wanataka kujitathmini na kukirudisha chama hicho kusimamia misingi iliyoanzishwa na waasisi wake kuwa chama cha kupigania na kusimamia maslahi ya wanachama wake na wananchi na siyo kuwa kimbilio au kuwa kichaka cha watenda maovu.
Akizungumzia maagizo hayo Katibu wa uenezi, Siasa na Mafunzo CCM mkoa Kigoma, Deogratius Nsokolo amesema kuwa wamepokea maagizo hayo na utekelezaji utaanza haraka iwezekanavyo kwani hilo ni jambo la msingi katika kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za chama.
Nsokolo alisema kuwa mwakani ni mwaka wa uchaguzi ndani ya CCM hivyo katiba inapaswa kufahamika kwa wanachama wote ili kuufanya uchaguzi wa kuwa wa kidemokrasia na unaozingatia misingi ya haki.







0 Comments