Na WILLIUM PAUL, VUNJO.
MBUNGE wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, amefanya ziara rasmi katika Ofisi ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), kwa lengo la kujitambulisha pamoja na kupata taarifa za kina kuhusu utendaji wa hifadhi hiyo na namna inavyoshirikiana na jamii zinazozunguka hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
Ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa, ambapo uongozi wa KINAPA ulitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizoulizwa na Mbunge, pamoja na maelezo kuhusu shughuli za uhifadhi, changamoto zilizopo na mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya hifadhi na wananchi wa maeneo jirani.
Mheshimiwa Mbunge aliambatana na Madiwani kutoka kata zinazopakana na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro upande wa Vunjo, wakiwemo, Innocent Melleck Shirima, Diwani wa Kata ya Marangu Mashariki, Heriel Ngowi, Diwani wa Kata ya Kirua Vunjo Magharibi, Leonard Ngowi, Diwani wa Kata ya Mamba Kaskazini na Anna Lyimo, Diwani wa Kata ya Kilema Kaskazini
Kwa upande wa KINAPA, ujumbe uliongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, Angel Nyaki, akiambatana na viongozi waandamizi na wataalamu wa hifadhi hiyo.
Mbunge alieleza kuridhishwa na maelezo aliyopata na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya KINAPA, viongozi wa serikali za vijiji na wananchi ili kulinda mazingira, kukuza utalii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa jamii zinazozunguka hifadhi.
Mwisho..








0 Comments