Header Ads Widget

DC MONGELLA AONGOZA UPANDAJI MITI KALIUA, TFS YATOA MICHE 3,500


Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mhe. Dkt. Gerald Mongella, Januari 6, 2026 ameongoza zoezi la upandaji miti katika mji wa Kaliua, akisisitiza umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kama nguzo ya maendeleo endelevu na ustawi wa jamii.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo lililofanyika kando ya barabara ya Kasungu kuanzia mjini Kaliua, Dkt. Mongella aliwataka wananchi, taasisi za umma na binafsi kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa ipasavyo kwa kuweka kingo za ulinzi ili isiharibiwe na wanyama, huku akihimiza uendelevu wa jitihada za uhifadhi.

Katika zoezi hilo la leo, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilayani Kaliua ulitoa na kushiriki kupanda pamoja na kugawa miche ya miti 3,500 kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha misitu ya mijini (urban forest) na kuongeza uoto wa asili katika maeneo ya makazi.




Akizungumza kwa niaba ya Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilayani Kaliua, CR. I Mustapha Msangi alisema zoezi hilo lina lengo la kuimarisha na kuhamasisha uhifadhi wa misitu mijini sambamba na kujenga ari ya wananchi katika kuthamini miti kama rasilimali muhimu kwa maisha na uchumi.

Aliongeza kuwa, miche 2,500 ilipandwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kando ya barabara ya Kasungu, huku miche 1,000 ikigaiwa kwa taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wengine, akiwemo Hospitali ya Wilaya ya Kaliua na wafanyabiashara, kwa ajili ya kupandwa katika maeneo yao.

Alitaja aina za miche iliyopandwa na kugaiwa kuwa ni pamoja na Misederela, miti maji, mijohoro na miti ya matunda, ikiwa ni mchanganyiko unaolenga kuboresha mandhari ya mji, kuimarisha ikolojia na kuongeza manufaa ya kijamii na kiuchumi kwa jamii.

Zoezi hilo lilishirikisha watumishi wa TFS Kaliua kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, chini ya usimamizi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, ikiwa ni utekelezaji wa sera na mikakati ya taifa ya uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI