Na WAF, Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kutoka kiwango cha chini (Level 1) mwaka 2016 hadi viwango vya juu (Levels 3 na 4) mwaka 2024, katika utekelezaji wa mpango wa Taifa wa mapambano dhidi ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (UVIDA).
Dkt. Nchini ametoa kauli hiyo leo Desemba 3, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua wiki ya kupambana na changamoto ya UVIDA inayo wakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.
Dkt. Nchimbi amesema Tanzania imeweka kipaumbele cha mapambano ya UVIDA kupitia afua mbalimbali zilizoainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Kukabiliana na UVIDA (2023–2028) kwa kutumia mtazamo shirikishi wa (One Health) kwa kuzikutanisha kwa pamoja sekta za afya, mifugo na kilimo kushughulikia changamoto hiyo, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ahadi za Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa za mapambano dhidi ya UVIDA.
Mbali na hatua kubwa ambayo tayari imepigwa ameutaka mkutano huo kutekeleza mambo sita muhimu ambayo endapo watafanikiwa kwa kuweka nguvu za pamoja basi huenda tatizo hilo la usugu wa vimelea likatokomezwa kabisa.
"Niwatake muongeze uelewa na elimu kwa umma kuhusu UVIDA, muimarishe ufuatiliaji wa matumizi ya dawa na usugu, jambo lingine ni mpanue hatua za kinga katika hospitali, mashambani na kwenye jamii," amesema Dkt. Nchimbi.
Makamu wa Rais Nchimbi ameutaka Mkutano huo kutilia mkazo masuala ya kukuza matumizi sahihi ya dawa kwa binadamu, mifugo na mazao, kusimamia kisheria udhibiti wa matumizi mabaya ya dawa na kuhakikisha tafiti, bunifu na njia mbadala za matibabu vinapewa kipaumbele.
Awali akitoa Salam za Wizara Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa ameainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa mpango huo, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa mifumo ya maabara, usimamizi bora wa matumizi ya dawa na uboreshaji wa huduma za kinga ya maambukizi katika vituo vya afya.
"Hatua hizi zimeiwezesha Tanzania kutekeleza kwa ufanisi ahadi zake za kimataifa, hususan zile zilizotolewa katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu AMR," amesema Mhe. Mchengerwa.
Mkutano wa bara la Afrika kuhusu kukabiliana na Usugu wa Vimelea vya magonjwa unafanyika Tanzania unaongozwa na Kaulimbiu isemayo chukua hatua sasa, ilinde leo na kesho yako.




















0 Comments