Header Ads Widget

SERIKALI YADHAMIRIA KUWAINUA WAKULIMA WA ZAO LA PAMBA NCHINI KWA KUTOA VIWATIRIFU.

 

Mashaka Mashimba, Mratibu wa Zao la Pamba,  Halmashauri ya Wilaya ya Bunda akielezea namna boza za kisasa zenye uwezo wa kubeba lita 300 za dawa na inavyoweza kumsaidia mkulima kupulizia shamba kwa haraka na ufanisi.

Na Chausiku Said 

Matukio Daima.

Serikali kupitia bodi ya pamba imedhihirisha jitihada kubwa katika kuhakikisha kuwa wakulima wa zao la pamba wanakabiliana na changamoto za viwadudu waharibifu, ambao wamekuwa wakishambulia mashamba na kupunguza tija ya uzalishaji wa zao hilo Kwa kutoa viwatirifu, matrekta na teknolojia nyingine za kisasa.

Katika kuhakikisha zao la pamba kinakuwa na tija serikali imeendelea kuwa mstari wa mbele kuwasaidia wakulima wa zao hilo kupitia usambazaji wa viwatirifu na vifaa vya kisasa vya kupulizia. Kwa msimu huu, bodi ya pamba imekuwa ikitoa viwatirifu vya kisasa kwa wakulima, ikiwa ni pamoja na dawa za kuzuia wadudu mafuta, chawajani, vitumba, na kanga mbili, ambao ni baadhi ya viwadudu waharibifu wakuu katika kilimo cha pamba

Mashaka Mashimba, Mratibu wa Zao la Pamba,  Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Katikati akiwarlekeza wakulima namna ya kunyunyuzia dawa ili kuwauwa wadudu waharibifu katika zao la pamba.

Mkama Bugarika, Mkulima kutoka Kijiji cha Bulendabufwe, kata ya Igundu Wilaya ya Bunda Mkoani Mara ameeleza kuwa  viwatirifu hivyo vimekuwa msaada katika kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao hilo la pamba pia serikali imewazesha wakulima kupata huduma hizo  muhimu za kupambana na wadudu hatarishi, jambo ambalo linapunguza hasara kubwa inayoweza kutokea.

“Mwaka huu, serikali Kwa kushirikiana na bodi ya pamba imetuuletea viwatirifu bora na huduma za unyunyuziaji wa dawa mashambani mapema, hii itakuwa na manufaa makubwa kwetu kuhakikisha tunapulizia mapema dawaili kupunguza maambukizi ya wadudu waharibifu,” alisema Bugarika.

Mkama Nyahonge, mkulima kutoka Kijiji cha Bulendabufwe, akielezea jinsi viwatirifu hivyo vimekuwa msaada katika kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao hilo la pamba.

Mratibu wa Zao la Pamba Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mkoani Mara Mashaka Mashimba ameeleza kuwa mbali na serikali kutoa viwatirifu pia  imeanzisha matumizi ya teknolojia ya kisasa kama matrekta, boza na drones ili kusaidia wakulima kudhibiti viwadudu kwa ufanisi. 

Mashimba amefafanua kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ilipokea matrekta 25 kutoka bodi ya pamba, ambayo yanatumika kwa ajili ya kuandaa mashamba, kwani uwepo wa vitendea kazi hivyo vimeweza kuwarahisishia wakulima kulima kwa haraka, na hivyo kuzuia wadudu kama vitumba kushambulia pamba.

Paschal Magesa, Afisa Kilimo kutoka Kata ya Igundu akielezea namna ambavyo wamekuwa wakitoa elimu Kwa wakulima kuhusu namna bora ya kutumia viwatirifu na vifaa vya kupulizia dawa.

Hata hivyo ameeleza kuwa Serikali imetoa boza za kisasa za kupulizia dawa, ambazo zina uwezo wa kubeba lita 300 za dawa na kumsaidia mkulima kupulizia shamba kwa, muda mfupi na Kwa ufanisi zaidi Vilevile, matumizi ya drones, ambayo yameleta suluhu kwa wakulima katika maeneo ya mbalimbali.

“Boza hizi ni za kisasa na zinatusaidia kupulizia dawa kwa urahisi na haraka, ili kudhibiti viwadudu waharibifu. Tumekuwa na matokeo mazuri kwa kutumia vifaa hivi, lakini pia kutumia drones, tunaweza kupulizia dawa kwenye mashamba ambayo ni vigumu kufikiwa na boza au matrektai imeongeza ufanisi wa kudhibiti viwadudu,” alieleza Mashimba.

Paschal Magesa, Afisa Kilimo kutoka Kata ya Igundu Wilaya ya Bunda, amesema kuwa Serikali kupitia maafisa ugani wameendelea kutoa elimu kwa wakulima  namna bora ya kutumia viwatirifu na vifaa vya kupulizia dawa, hivyo kuwa wakulima wa zao la pamba kuendelea kushirikiana na maafisa ugani ili kupata maelekezo kuhusu matumizi sahihi ya viwatirifu na dawa za viwadudu.

“Maafisa ugani wanasaidia wakulima kuelewa namna ya kutumia viwatirifu ili kupata matokeo bora. Hii ni muhimu ili kuhakikisha kwamba tunatumia dawa sahihi kwa wadudu maalum na kupunguza madhara kwa mazingira,” alisema Magesa.


Kaliba Mkama, Mkulima kutoka Kijiji cha Bulendabufwe akielezea namna walivyoweza kunufaika na Teknolojia katika zao la pamba.

Kaliba Mkama, mkulima kutoka Kijiji cha Bulendabufwe, alieleza kuwa licha ya changamoto, matumizi ya viwatirifu vya kisasa yameleta mabadiliko makubwa. 

“Kwa msaada wa serikali, tunapata viwatirifu bora na teknolojia ya kisasa kama drones na boza za kisasa ambazo zimeongeza ufanisi katika kilimo chetu cha pamba,” alisema Mkama.

Aidha Kwa upande mwingine Mashimba ametos wito kwa wakulima wa pamba katika Wilaya ya Bunda na maeneo mengine kuendelea kutumia viwatirifu, boza, na drones zilizotolewa na serikali ili kudhibiti viwadudu waharibifu kwani  kutumia teknolojia ya kisasa ni muhimu ili kuongeza tija na kuhakikisha mavuno bora.

“Serikali imejitahidi sana kutoa msaada kwa wakulima katika vita dhidi ya viwadudu Sasa ni jukumu letu kama wakulima kutumia vyema rasilimali hizi ili kufanikisha kilimo cha pamba chenye tija,” alisema Mashimba.

Licha ya juhudi za serikali, changamoto ya viwadudu waharibifu bado ipo. Wadudu kama vitumba, chawajani, na wadudu mafuta wanazidi kuwa tishio, hasa wakati wa mvua chache au mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, serikali imesisitiza kuwa itaendelea kufanya kazi na wakulima na wadau mbalimbali katika kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kilimo, viwatirifu, na elimu ya kilimo bora.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI