Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
VIONGOZI wa dini nchini wametakiwa kuendelea kuhamasisha amani na kukemea wanaoleta chokochoko za kuvuruga umoja wa watanzania.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima alitoa wito huo alipomwakilisha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,wakati wa misa ya kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini Askofu wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro Dk George Pindua, pamoja na msaidizi wa askofu Peter Makalla
Malima alisema viongozi wa dini pamoja na kukemea wasichoke
kufundisha na kuhubiri amani kwa waumini wao na watanzania wote.
"Msichoke kufundisha maadili na kukemea mambo ya ajabu ajabu yanayotaka kuingia kwenye jamii yetu, kuna watu wanaingia kwenye jamii yetu kwa makusudi kabisa na kutumbukiza mambo mengine ambayo sisi hatuna,"alisema Malima.
"Waislamu, wakristo na hata wasio na dini, watanzania hatuna tabia hizo.... Ukishaona mtu amekuja na kuna vipesapesa vinaingia na anahamasisha ndoa za jinsia moja na maandamano ujue hapo kuna tatizo,"alisema Malima.
Alizitaka taasisi za dini kuendelea kushirikiana na serikali katika mambo ya kijamii ikiwemo masuala ya mazingira, afya na elimu .
Mkuu wa mkoa huyo aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ibada hiyo aliwasilisha pia mchango wa shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya kijamii inayotekelezwa na KKKT Dayosisi ya Morogoro.
Akizungumza mara baada ya kuwekwa wakfu, Askofu Dk Pindua alisema ili kuweza kutoa huduma bora kwa jamii KKKT dayosisi ya Morogoro inaiomba serikali kuwaunga mkono kwa kuwaletea wataalamu wa afya, vitanda na vifaa tiba.
"Ili kutoa huduma bora kwa jamii tunaomba serikali ituunge mkono kwa kuimarisha kituo cha afya Mkulazi ikiwa ni pamoja na kutupatia madaktari, kuboresha wodi ya akina mama wajawazito na watoto kwani ili kukamisha yote hayo zinahitajika zaidi ya sh milioni 200,"alisema Dk Pindua.
Aliongeza kuwa KKKT dayosisi ya Morogoro imekuwa kinara wa kupinga ukatili dhidi ya ya watoto wa kike ikiwemo ndoa za utotoni, vitengo vya ulawiti na ubakaji ndani ya mkoa kwa lengo la kutunza heshima na utu wa binti wa kitanzania.
Alisema wasichana wadogo wamekuwa wakikatishwa masomo na kulazimishwa kuolewa wakiwa na umri mdogo.
"KKKT kwa kushirikiana na wadau wamejenga kituo cha kusaidia kuwahifadhi mabinti wanaokatishwa masomo na kulazimishwa ndoa za utotoni na baadae kupatiwa huduma za kisheria na kufanikiwa kurudi masomoni,"alisema Dk Pindua.
Mkuu wa kanisa la kiinjili la kilutheri (KKKT) Tanzania Dk Alex Malasusa aliwataka watanzania kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano na kuwaasa waumini kuacha kufuata mkumbi kwa mambo yasiyofaa na kuiombea amani Tanzania
KKKT Dayosisi ya Morogoro ina zaidi ya waumini 45,000,katika ibada hiyo viongozi mbalimbali wa Serikali walishiriki akiwemo naibu Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Denis Londo, naibu Waziri mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki James Ole Milya pamoja na mbunge wa Morogoro mjini Abdullaziz Abood.
Mwisho..








0 Comments