Bi. Pili Ndimanya Mkazi wa Mvuti Wilayani Ilala Mkoani Dar Es Salaam amelaani matukio ya uharibifu, wizi na ghasia zilizojitokeza Oktoba 29, 2025 kwenye maeneo mbalimbali nchini, akiwataka Vijana kujitafakati na kuchukua hatua za kutorubuniwa tena na kuwa sababu ya kuharibu amani.
Pili Ndimanya amebainisha hayo ikiwa zimepita siku chache tangu kutolewa kwa tamko la msamaha kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan Bungeni Mjini Dodoma, akizitaka mamlaka za sheria nchini kuwaachilia wale wote watakaobainika kuwa walifuata Mkumbo na kufanya vurugu siku hiyo ya uchaguzi Mkuu.
Bi. Pili amebainisha kuwa tangu kuzaliwa kwake hakuwahi kushuhudia uharibifu na vurugu kubwa kama zilizotokea Jumatano ya Oktoba 29, 2025, akisema yale hayakuwa maandamano kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakieleza kwenye majukwaa mbalimbali.
"Wito wangu mkubwa naomba watoto wetu wote na Vijana wote mliotoka barabarani siku ile mjiulize aliyewatuma alikuwepo barabarani? Nani kaathirika? Ni muhimu mtumie njia nzuri kuwasilisha kero zao, mimi naomba watu wabadilike na waachane na hila za kuiharibu nchi yetu."
Amesisitiza kuwa wapo wengi wasioipenda amani ya Tanzania na ni muhimu kuwafahamu na kujiepusha nao, akiwataka kurejea uzoefu wa wengi katika kipindi cha takribani siku tano tangu Oktoba 29, 2025 na athari walizozipata hasa baada ya kushindwa kutoka nje na kuendelea na shughuli zao za kujitafutia kipato kuendesha maisha yao kama ilivyokuwa.





0 Comments