Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Cha Sokine Cha Kilimo SUA Andrew Massawe, akiwa na naibu makamu mkuu wa Chuo Kikuu Cha Sokine Cha Kilimo SUA Profesa Amandus Muhairwa, alipotembelea Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi.
Matukio DaimaApp
MWENYEKITI wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Andrew Massawe, ametembelea Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi na kukagua maendeleo ya miradi ya miundombinu inayotekelezwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Ziara hiyo ya mwenyekiti wa Baraza SUA pia ililenga kuimarisha ushirikiano kati ya SUA na jamii ya eneo husika pamoja na kujadili mikakati ya kukuza elimu ya kilimo katika maeneo ya pembezoni.
Kupitia ziara hii, SUA imeonesha dhamira yake ya dhati ya kuendeleza elimu bora, ubunifu, na tafiti zenye tija kwa maendeleo ya taifa, hususan katika sekta ya kilimo ambayo ndiyo mhimili wa uchumi wa Tanzania.
Massawe alipata fursa ya kuzungumza na wakuu wa idara na vitengo mbalimbali vya kampasi, ambapo walijadili maendeleo ya kampasi na mikakati ya kuimarisha utoaji wa elimu ya vitendo kwa wanafunzi.
Aidha, alitembelea maeneo ya hekari 689 yaliyotwaliwa na chuo kwa ajili ya upanuzi wa kampasi hiyo, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa SUA katika kutoa huduma bora za kitaaluma na kijamii.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti Massawe alikagua maendeleo ya ujenzi wa majengo mawili muhimu, Jengo la Taaluma na Jengo la Bweni, yanayotekelezwa chini ya Mradi wa HEET kupitia Kampuni ya TIL Construction.
Akapongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, akibainisha kuwa uwekezaji huo ni msingi wa kuinua ubora wa elimu ya kilimo kwa vitendo na kuongeza fursa za ujifunzaji bora.
Akizungumza na viongozi wa kampasi, mwenyekiti Massawe alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi ya HEET inatekelezwa kwa ubora wa hali ya juu, ikizingatia dhamira ya serikali ya kuimarisha vyuo vikuu kuwa vyanzo vya maarifa, ubunifu na suluhisho za changamoto za kijamii na kiuchumi.
Aidha, alitoa pongezi kwa uongozi wa Kampasi ya Mizengo Pinda kwa usimamizi bora wa miradi ya maendeleo na kwa kuendelea kushirikiana na jamii katika shughuli za kilimo na utafiti.
Ziara ya Mwenyekiti wa Baraza la SUA katika Kampasi ya Mizengo Pinda imeonesha kwa vitendo mchango wa Mradi wa HEET katika kuboresha miundombinu, kukuza ubora wa elimu, na kuimarisha ushirikiano kati ya chuo na jamii.
Ni hatua muhimu kuelekea kujenga taifa lenye uwezo wa kujilisha, kubuni, na kushindana katika soko la kimataifa kupitia sekta ya kilimo







0 Comments