Na Samwel Mpogole – Mbeya
Jamii imetakiwa kujitokeza kwa wingi katika kuwasaidia watoto wenye uhitaji, hususan wale wanaoishi katika mazingira magumu, wakati viongozi wa taasisi za kijamii wakiendelea kuongoza harakati za kuwafariji na kuwapatia mahitaji ya msingi.
Wito huo umetolewa katika tukio maalumu la kutembelea watoto wenye changamoto mbalimbali, ambapo Mkurugenzi wa Umoja wa Marafiki na Urafiki, Joaz Mguta, ameongoza wanachama wa umoja huo katika kutoa faraja, msaada na matumaini mapya kwa watoto hao.
Mguta amesema kuwa ni wajibu wa kila mwanajamii kuhakikisha mtoto analelewa kwa upendo, analindwa ipasavyo na anapatiwa mahitaji muhimu bila kujali changamoto zinazomzunguka. Amesisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni nguzo muhimu katika kujenga kizazi chenye matumaini na uwezo wa kutimiza ndoto zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Funguka Foundation, Bi. Nelly Elisha, taasisi inayohudumia watoto wenye ulemavu, yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi, amesema bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika kutoa huduma. Ametoa mfano wa kukatiwa huduma ya maji baada ya bili kufikia zaidi ya shilingi laki tatu, hali ambayo imekuwa mzigo kutokana na majukumu mengi ya kuwatunza watoto.
Ameeleza kuwa zaidi ya watoto 70 wanategemea huduma za taasisi hiyo, hivyo kuna uhitaji mkubwa wa msaada katika lishe, afya, vifaa vya shule na mahitaji mengine muhimu ili kuhakikisha ustawi wao unabaki kuwa kipaumbele. Ameitaka jamii na wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuunga mkono jitihada hizo.
Baadhi ya washiriki wa tukio hilo wamesema juhudi zinazofanywa na taasisi hizo zinastahili kuungwa mkono kwa kuwa zinaboresha maisha ya watoto wanaokabiliwa na changamoto.
Wamehimiza watu wenye uwezo kujitoa kwa moyo wa upendo ili kusaidia mustakabali wa watoto hao na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.









0 Comments