Header Ads Widget

HUDUMA YA MWENDOKASI YASITISHWA KUPISHA TATHMINI YA UHARIBIFU ULIOFANYIKA OKTOBA 29.

 


Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Albert John Chalamila ametangaza kusitisha huduma za usafiri wa mabasi yaendayo haraka maarufu kama mwendokasi kati ya Gerezani - Kimara na Gerezani - Mbagala Jijini Dar Es Salaam.

Kusitishwa kwa huduma hiyo kulingana na Mhe. Chalamila katika Taarifa yake kwa Vyombo vya habari, kunalenga kutoa nafasi ya kufanyika kwa tathmini ili kujua uharibifu uliofanyika wakati wa maandamano yaliyofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 jijini Dar es Salaam.

Katika maandamano hayo, waandamaji waliharibu miundombinu hususan vituo vya mwendokasi, zaidi katika vituo vilivyopo barabara ya Morogoro kwa kuvunja vituo, mifumo ya ukataji wa tiketi na kuvichoma moto baadhi ya vituo vya kushusha na kupakia abiria.

Chalamila katika taarifa yake amewataka wananchi wote waliokuwa watumiaji wa usafiri huo kutafuta njia mbadala za usafiri katika kipindi hiki wakati ambao unafanyika utaratibu wa kurudisha hali kama ilivyokuwa awali.

“Tunasitisha mara moja usafiri huu ili kufanya tathmini ya kina ya uharibifu uliotokea kwani mifumo ya ukataji tiketi imeharibiwa jambo ambalo linahitaji muda ili kurudisha hali kama ilivyokuwa awali,” amesema Chalamila.

Mkuu huyo wa Mkoa katika hatua nyingine amewaagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini LATRA kutoa vibali vya muda mfupi kwa mabasi ya kawaida ili yaweze kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji kwenye njia hizo ambazo zilikuwa zikitegemea mabasi ya mwendokasi yaliyosimama kutoa huduma katika barabara tajwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI