Header Ads Widget

VIONGOZI WA DINI SINGIDA NA DODOMA WAHIMIZA VIJANA KULINDA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Na Hamida Ramadhan, MatukioDaimaMedia Dodoma

VIONGOZI wa Dini kutoka mikoa ya Singida na Dodoma wamewataka vijana kuepuka vishawishi vya vurugu na mifarakano ya kisiasa, wakisisitiza kuwa kulinda amani ni jukumu la kila Mtanzania kadri Taifa linavyoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.


Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma katika kongamano la viongozi wa dini mbalimbali kutoka Kanda ya Kati, lililolenga kuliombea Taifa amani na utulivu kuelekea uchaguzi huo.


Akizungumza katika kongamano hilo, Askofu Evance Chande wa Kanisa la Carmel Assemblies of God amesema vijana wanapaswa kutumia nguvu zao katika kujenga Taifa badala ya kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi.


“Tunapaswa kuikumbatia amani kama tunavyokumbatia imani zetu. Uchaguzi ukipita, Tanzania inabaki kuwa moja. Tusikubali kugawanywa kwa misingi ya kisiasa,” amesema Askofu Chande.


Kwa upande wake, Sheikh Mustapha Rajab, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Kanda ya Kati, ambaye pia alikuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo, aliwahimiza wananchi kutii mamlaka na kufuata sheria pamoja na taratibu zinazotolewa na Serikali na viongozi wa dini.

 “Amani si jambo la bahati mbaya; ni matokeo ya utii na hekima tukitii viongozi wetu na kuheshimu sheria, Taifa litaendelea kubaki salama,”

amesema Sheikh Rajab.

Kongamano hilo lilifanyika chini ya kaulimbiu isemayo:

“Kupiga kura ni haki ya kila Mtanzania; amani na utulivu ni jukumu letu.”

Viongozi hao walisisitiza kuwa kulinda amani si wajibu wa Serikali pekee, bali ni jukumu la kila raia, huku wakihimiza maombi, maelewano na uvumilivu kama silaha za kudumisha utulivu wa Taifa wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi

















Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI