Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekana madai kwamba ukandamizaji wa kisiasa umeongezeka nchini humo wakati taifa hilo linapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akijibu ripoti iliyotolewa na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW), kuhusu madai hayo, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa amesema, taarifa hiyo sio sahihi na inapotosha .
Aidha Msigwa amepuuzilia mbali madai ya taarifa za kutekwa kwa raia nchini humo.
" Madai kuwa kuna kupungua kwa uhuru wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 si ya kweli," Taarifa hiyo imesema.
"Katiba ya nchi inatoa haki ya kuishi, usalama na uhuru kwa kila Mtanzania," Taarifa hiyo imeongeza.
Msemaji huyo amelilaumu shirika hilo kwa kutoa taarifa za aina hiyo bila kuipatia serikali fursa ya kujibu .
Msigwa amesema serikali ya Tanzania ipo tayari wakati wowote kushirikiana na taasisi yoyote inayotafuta taarifa sahihi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya HRW, mamlaka ya Tanzania imekandamiza upinzani na wakosoaji wa chama tawala, kunyamazisha vyombo vya habari, mbali na kushindwa kuhakikisha uhuru wa tume ya uchaguzi.
Nomathamsanqa Masiko-Mpaka, mtafiti wa Afrika katika Human Rights Watch alisema:
"Mamlaka inahitajika kujizuia kukandamiza upinzani na vyombo vya habari, na badala yake hushiriki katika mageuzi wenye maana ili kuhakikisha unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika,".
Aidha Ripoti hiyo imetoa wito kwa serikali ya Tanzania kuchukua hatua za haraka kulinda uadilifu wa uchaguzi mkuu ambao HRW imedai uko katika hatari kubwa .
Tanzania imesema kuwa imejipanga kuhakikisha haki za binadamu, demokrasia, utawala bora na sheria vinaheshimiwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.






0 Comments