Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio Daima Media
WAKULIMA wa kijiji cha Pemba, wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro walioanza kulima miti ya asili kwa lengo la kulinda hifadhi na milima Nguu iliyoharibiwa na shughuli za kibinadamu na kujiandaa kuingia kwenye biashara ya hewa ukaa, wameanza hatua za awali za kujiandikisha kuwa walipa Kodi baada ya kufahamu umuhimu wake.
Hatua hiyo iliyoanza kwa kujiandikisha na kupata vitambulisho vya Taifa (NIDA),ili baadaye kujisajili kupata namba ya mlipa Kodi(TIN), itawezesha kushiriki ulipaji wa kodi kwa manufaa ya maendeleo yao na taifa Kwa ujumla.
Baadhi ya waandishi wa habari akiwemo mwandishi wa Habari hii walifika kijijini hapo, umbali wa zaidi ya Kilometa 150 kutoka mjini Morogoro na kuzungumza na wananchi waliofurahia hatua hiyo na kueleza manufaa watakayopata.
"Zamani tulijua masuala ya ulipaji Kodi ni kwaajili ya Watumishi wa Serikali, wafanyabiashara wakubwa, na watu wa mjini tu, lakini kumbe hata Mimi mkulima wa kawaida wa miti huku vijijini Nina nafasi ya kulipa kodi, tayari najua umuhimu wa Kodi kwa maendeleo yetu wenyewe,"alisema Flora Ramadhan, mmoja wa wananchi wa Kijiji Cha Pemba.
Wananchi wengine waliozungumza ni Aloyce Joseph ,Victoria Charles kwa nyakati tofauti walisema wanaamini kodi watakayolipa itarudi tena kwao kijijini kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo miundo mbinu ya barabara, huduma za afya, shule na huduma nyingine za kijamii.
"Zamani mambo mengi yalitupita, hata NIDA hatukuwa nazo,huu umekuwa mwanzo mzuri nasi kutambuliwa kama walipa Kodi,"aliongeza Michael Joseph, Mkazi wa Kijiji hicho cha Pemba.
Mratibu wa mradi wa Pams Foundation, waliowezesha wananchi hao kuanza kupanda miti ya asili kwa hiyari kando kando ya Milima Nguu wakiwapatia miche bure na huduma za kuandaa na kupalizi mashamba ya miti, Richard Paul alisema tayari wamefanikisha kuwaandikisha wakulima wa miti zaidi ya 350 Kati ya 1000 waliowakusudia kuwa na NIDA.
Aklisema hatua hiyo ni kuwezesha ili waweze kurasimishwa katika mfumo wa kodi kupitia TIN na kwamba mwamko wa uandikishaji ni mkubwa.
Meneja msaidizi wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro, anayeshughulikia Huduma kwa mlipa Kodi Chacha Boaz Gotora alisema kodi zitakazolipwa na wakulima hao zitasaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Eneo hili na hewa ukaa ni eneo jipya la kikodi kwa mkoa wa Morogoro, niyapongeze mashirika na taasisi wanaohamasisha wananchi kulipa kodi, Kwa sasa mashirika yakiwemo ya kimataifa yanayofanya kazi na wananchi kama Pams wamekuwa wakilipa Kodi ya zuio.
Gotora alisema hiyo ni Kodi wanayoizuia wakati wakilipa malipo mbalimbali kwa wananchi, lakini hatua ya kuwahamasisha kuwa na namba ya mlipa Kodi yaani TIN ni muhimu kwani inamtambua rasmi mlipa Kodi naye anaona mchango yake anayotoa na faida nyingine nyingi.
Alisema kwa mwamko wa wananchi wa Pemba hasa wakulima wa miti, watawafikia kwa karibu kwa kuwasogezea huduma ya elimu na usajili, na kwamba ukiwa na NIDA ni rahisi kwa yeyote kujisajili TIN mtandaoni.
Mwisho.








0 Comments