Header Ads Widget

COPRA WAKABIDHI MBEGU ZA CHOROKO SIMIYU.




Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.


WAKULIMA wa zao la Choroko Mkoani Simiyu wamenufaika na Tani tatu za Mbegu aina ya Imala kutoka Mamlaka ya udhibiti Nafaka na mazao  mchanganyiko (COPRA) ambazo zitagawiwa bure kwa wakulima.


Mkuu wa Mkoa huo Anamringi Macha amekiri kupokea Mbegu hizo za choroko tayari  kwa ajili ya kusambazwa bure kwa wakulima wa zao la Choroko katika Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu.


Akizungumza wakati wa  hafla ya makabidhiano ya mbegu hizo Ofisini kwake Nyaumata, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Macha ameishukuru Serikali kwa jitihada mbalimbali zinazofanywa kumuinua Mkulima.


Amewataka wakulima watakaonufaika na mbegu hizo kuzitumia kwa malengo ya uzalishaji badala ya kutumia kama chakula  kwa kua mbegu hizo zimehifadhiwa na viuadudu ambavyo ni hatari kwa Afya ya binadamu.




Aidha ameziagiza Halmashauri Mkoani humo kuhakikisha kuwa Mbegu hizo zinasambazwa kwa walengwa waliokusudiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Operesheni na udhibiti  ubora wa COPRA Kamwesege Mutembei amesema Mbegu hiyo aina ya Imala  ni kwa ajili ya wakulima ambao waliuza mazao yao kupitia mfumo wa Stakabadhi mazao ghalani na kwamba mfumo wa kidigitali utatumika kwa ajili ya ugawaji wa mbegu hizo.




Naye Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya uchumi na uzalishaji Juma Saidi Topera amewahakikishia COPRA kuwa Mbegu hizo zitagawiwa kwa utaratibu kwa usimamizi wa karibu wa Maafisa Ugani wa Halmashauri na kwamba zitawafikia wakulima kama ilivyokusudiwa.


Mwisho.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI