MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) CAG Msataafu Profesa Mussa Juma Assad, akizungumzia hali ya ukuaji wa uchumi nchini.Na Lilian Kasenene, Morogoro Matukio DaimaApp
MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) CAG Msataafu Profesa Mussa Juma Assad, amelinganisha hali ya uchumi ya sasa na kipindi cha nyuma akisema katika kipindi cha miaka minne uchumi umekuwa kwa asilimia sita na mfumuko wa bei upo katika hali nzuri.
Profesa Assad alisema hayo kwenye Kongamano la kitaaluma la kujadili Utekelezaji wa Uchumi Jumuhishi kufikia Dira 2050, lililoandaliwa na MUM kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi(PPPC) mjini Morogoro.
Profesa Assad alisema hata kwa vigezo vya kawaida uwezo wa watu ni kwa kipindi hiki cha miaka minne ni mzuri kwakuwa watu wanaweza kuishi maisha yao kwa ujumla wake uchumi wa Tanzania ni mzuri kwa vigezo vya kiuchumi ukilinganisha na nchi za Kenya na Rwanda.
“Kwa jumla Uchumi wa Tanzania umekuwa kwa wastani wa asilimia sita, GDP, kupanda na kushuka kwa pato la Taifa kumekaa vizuri ukilinganisha na nchi jirani,“alisema Profesa Assad.
Akizungumzia kuhusu uchumi jumuishi, Profesa Assad alisema, katika kipindi cha miaka 25 ijayo linatakiwa lifanywe kwa dhamira kubwa ili kila mmoja aingizwe kwenye uchumi jumuishi.
Profesa Assad alitolea mfano kuwa vijana wengi wanaomaliza Vyuo vikuu hawana ujuzi wa kutenda mambo na kwamba tatizo sio uchumi hauwaingizi bali wenyewe hawana ujuzi hivyo kuna haja ya vijana wanaohitimu wapewe ujuzi wa kutosha.
“Vijana tunaowatoa sasaivi tunapaswa kuwapa ujuzi baada ya kumaliza Vyuoni ni hiyo ni kazi ya Serikali na pia sekta binafsi kuwachukua na kuwafundisha kozi za muda wa miezi mitatu ili wanapohitimu wawe na kitu cha kufanya” alisema Profesa Assad.
Alisema kwa maoni yake bado ukusanyaji wa takwimu unatumia mifumo ya kizamani akitolea mfano matumizi ya makaratasi wakati kwenye ukusanyaji wa mapato wanatumia mfumo wa kidigiti hivyo kuna haja kutumia mfumo huo kwenye kutoa taarifa.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha PPPC, David Kafulila, akizungumza kwenye Kongamano hilo kuhusu tathimini ya uchumi katika kipindi cha miaka minne alisema wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani alikuta eneo la umwagiliaji hekta 540,000 lakini katika kipindi cha miaka minne eneo hilo limefikia hekta milioni moja.
Kwenye sekta ya Madini, Kafulila alisema ilikuwa ikisemwa na kulalamikiwa ni ya wachimbaji wakubwa na wageni lakini uhamuzi wa Rais wa kuzibadilisha Hati kubwa za wachimbaji wakubwa na kuwapa wachimbaji wadogo taklibani 2600, imepekelea mchango wa wachimbaji wadogo pato la madini kuongezeka kutoka asilimia 20 wakati anaingia madarakani hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2024.
“Hii imefanya ushiriki wa watu wa kawaida ambao ni wachimbaji wadogo kuweza kuwa sehemu ya sekta hiyo kubwa ya madini na kundokana na malalamiko kuwa ni sekta ya wageni na watu wenye mitaji mikubwa,”alisema Kafulila.
Kuhusu sekta umeme, Kafulila alisema Rais Samia lipoingia madarakani alikuta msongo unaosafirisha umeme ulikuwa na kilomita 6000 kwa miaka 60 iliyopita lakini kipindi cha miaka minne ameuongeza kwa kilomita 2000 ambayo nia silimia 30 ya kiasi ambacho kimetengenezwa kwa miaka 60.
Naye Mchumi, Mwanazuoni, Dk Bravious Kahyoza, alisema tangu mwaka 2021 uiano wa biashara na pato ghafi ulikuwa asilimia 27 na imefika asilimia 43 mpaka sasa ambayo inaonyesha fursa kuongezeka na watu wanafanya biashara.
Alisema sekta ya Umma kwenye ajira katika kipindi cha miaka iliyopita ilikuwa haifanyi vizuri lakini katika kipindi cha miaka minne iliyopita imeweza kuajiri zaidi ya 400,000 na katika nchi inazozunguka Tanzania hakuna nchi iliajiri kama ilivyofanya Tanzania.
“Katika kipindi cha miaka minne Tanzania imefanya vizuri kwenye sekta ya Umma upande wa ajira ukilinganisha na Kenya imeajili watu 311,000,Uganda watu 196,000 na Rwanda imeajili watu 20,000,” alisema Dk Kahyoza.
Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe ambaye Mtalaam wa PPP,Moshi Derefa,alisema duniani mfumo wa uwekezaji katika miradi mingi imeamia kwa kutumia mbinu za ubia kwa kushirikisha sekta binafsi ili kuweza kuchangia katika utekelezaji wa miradi kwa kutumia rasilimali fedha, teknolojia walizonazo na uzoefu walionao.
“Tuna imani na tunaelewa wenzetu sekta binafsi wanakuwa wako mbele kidogo katika mazingira hayo kwasababu unaposhirikisha sekta binafsi sio unashirikisha wadau kutoka ndani ya nchi lakini unashirikisha wadau au wawekezaji kutoka nje ya nchi ambazo zipo mbele zaidi kiteknolojia na kiujuzi kwa sekta mbalimbali,”alisema Moshi.
Mwisho.







0 Comments