Header Ads Widget

WANANCHI WAFUNGA OFISI YA KIJIJI MOROGORO

 

Na Lilian Kasenene, Morogoro

Matukio DaimaApp 

WANANCHI wa kijiji cha Bwakila Chini Wilaya ya Morogoro wamefunga ofisi ya kijiji hicho wakilalamikia kuuzwa kwa ekari 207 za ardhi kwa mwekezaji Morogoro Sugar bila ridhaa yao.


Mgogoro wa ardhi katika kijiji hicho umezidi kushika kasi ambapo wananchi hao wanasema mkataba wa mwaka 2018 unaodaiwa kusainiwa kati ya viongozi wa muda na mwekezaji huyo ni batili kwa kuwa haukushirikisha mkutano wa kijiji.


Wananchi hao wameibua madai ya ukosefu wa taarifa za mapato na matumizi, pamoja na kulipwa fidia kwa watu wasiokuwa na mashamba badala ya wamiliki halali.


“Tumenyang’anywa mashamba yetu kinyume cha sheria, tumetoa barua zaidi ya 400 kuomba mkutano wa kijiji lakini hatujapata majibu. Tunaamini Rais Samia atatusikiliza,” alisema Kibwana Hamis Hasira, mmoja wa wananchi.


.


Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hemed Mvunyo, alipoulizwa alisema mikutano ya kijiji hufanyika kila baada ya miezi mitatu na kudai suala la mkataba lipo kwenye vyombo vya sheria.


Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, alisema hatua ya kwanza ilikuwa kuhakikisha ofisi ya kijiji inafunguliwa ili huduma kwa wananchi ziendelee, na kwamba madai ya mkataba feki bado ni tuhuma zinazofuatiliwa

Hivi karibuni, mpima ardhi msaidizi wa wilaya, Kadofadha Marwa, alithibitisha kuwa ekari 2,580 za kijiji hicho pamoja na ekari 301 za wananchi tayari zilibadilishwa matumizi kisheria na kukabidhiwa kwa mwekezaji kwa ajili ya kilimo cha miwa.


Tayari watu kadhaa wanadaiwa kuendelea kukamatwa na Polisi kijijini hapo kwa tuhuma za kufunga ofisi hiyo ya Kijiji na kuletwa kituo Kikuu cha Polisi mjini Morogoro ambapo jitihada za kumpata Kamanda wa  Polisi mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama zinaendelea kujua idadi ya waliokamatwa, na makosa wanayoshtakiwa nayo na lini watafikishwa mahakamani.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI