Mamlaka ya uwekezaji na maeneo maalum ya uchumi nchini Tanzania (TISEZA) imeahidi kuendelea kudumisha mazingira ya wawekezaji wote wakiwemo wa ndani ya nchi ili kukuza uchumi katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Mamlaka hiyo imesema itazidi kuboresha na kuhamasisha uwekezaji kwenye maeneo maalum ya uchumi kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya uwekezaji wa wananchi.
Akizungumza kwenye maonyesho ya biashara ya kusini (International Trade Fair and Festival) yaliyofanyika kwenye fukwe za Matema wilayani Kyela mkoani Mbeya, afisa uwekezaji wa TISEZA Nyanda za juu kusini bi. Privata Simon, amesema kuna fursa mbalimbali za uwekezaji katika kanda hiyo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi, madini na sekta ya usafirishaji.
Privata, amesema mbali na fursa hizo, pia Serikali itaendelea kutoa vivutio kwa wawekezaji wanao hitaji kuwekeza kwenye maeneo maalum ya uwekezaji yaliyoainishwa ikiwa ni pamoja na kupewa ardhi bure punguzo la kodi, kupata vibali vya ujenzi kwa haraka (ndani ya saa 24) na fursa ya kuhudumiwa kwa haraka kupitia taasisi 16 za kituo cha pamoja.
Kwa upande wake afisa uhamasishaji wa wawekezaji kutoka mamlaka ya uwekezaji na maeneo maalum ya uchumi Tanzania bwana Custhbert Kangila, amesema TISEZA katika inaendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuhamasisha na kukuza uchumi wa Tanzania kupitia uwekezaji hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuungana na Serikali kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa shwari na kushirikiana vema na wawekezaji wanaokuja katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa baadhi ya wawekezaji wa ndani nchini Tanzania, juhudi za Serikali kupitia mamlaka hiyo inavyowasaidia wananchi kufikiwa na fursa mbalimbali za uwekezaji ni wazi kwamba inasaidia kufikiwa pia kwa malengo ya uwekezaji wa viwanda nchini Tanzania katika kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
0 Comments