Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MGOMBEA ubunge jimbo la Kigma Mjini Zitto Kabwe amewaomba wapiga kura katika jimbo hilo kumchagua kuwa mbunge kwani yeye ndiye mwenye funguo ya kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi wa jimbo hilo.
Kabwe alisema hayo alihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Kwa Kidagala kata ya Businde Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo alisema kuwa jimbo la Kigoma mjini linahitaji mtu shupavu ambaye atasimama imara kuhakikisha fedha inayopitishwa na serikali kwa ajili ya maendeleo ya watu wa mji huo inatolewa na miradi inatekelezwa.
Alisema kuwa akiwa Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini na wakati huo manispaa ya Kigoma Ujiji ikiwa na idadi kubwa ya madiwani kutoka chama cha ACT Wazalendo walifanya kazi kubwa kusimamia maendeleo ya mji huo ikiwa kusimama imara kuhakikisha mradi wa uboreshaji wa miji inatekelezwa na ndiyo maendeleo yanayoonekana sasa.
Aidha Mgombea ubunge huyo alisema kuwa akiwa Mbunge wa jimbo hilo kati ya mwaka 2015 hadi 2020 ndiyo aliyesimama kidete kupigania kutekelezwa kwa mradi wa soko la jioni maeneo ya Mwanga maarufu soko Marungu ambapo alikutana na Balozi wa Ubelgiji akampeleka eneo hilo na ndiyo fedha zikatoka kupiti mradi wa LIC na kubeza majigambo ya Mgombea wa CCM, Clayton Chipando maarufu baba Levo kuwa ndiye aliyesimamia soko hilo kuanzishwa.
Awali akiongea katika mkutano huo wa kampeni Mwenyekiti wa ngome ya vijana ACT Wazalendo, Abdul Nondo alisema kuwa kipindi cha uchaguzi ndiyo kinachoamua hatima ya maisha yao hivyo wasifanye makosa kwa kuchagua viongozi kwa mihemko bali waangali wagombea ambao watawatumikia na kushughulikia matatizo yao hivyo kuomba Zitto Kabwe achaguliwe kuwa Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini.
Naye Mgombea udiwani wa kata ya Kigoma Mjini, Hussein Kalyango alisema kuwa wakati Halmashauri inaongozwa na idadi kubwa ya madiwani wa ACT Halmashauri ilifanya kazi kubwa ya kusimamia maendeleo ya Mji wa Kigoma Ujiji hivyo ametaka wananchi kukichagua chama hicho kwa ajiili ya maendeleo yao.
Aidha katika mkutano huo Zitto Kabwe alikata keki na kuwalisha watu mbalimbali ikiwa ni ishara ya siku yake ya kuzaliwa akiwa ametimiza miaka 49 ambapo nyimbo mbalimbali za kumtakia heri ziliiambwa hapo jukwaani.
0 Comments