Header Ads Widget

GRACE TENDEGA AJITOSA KUSAKA KURA ZA KISHINDO ZA DKT SAMIA ,WABUNGE NA MADIWANI CCM

 


Na Matukio Daima Media, Kilolo

Aliyekuwa mtia nia wa ubunge Jimbo la Kalenga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Grace Tendega, ameungana na wagombea wa majimbo ya Kalenga na Kilolo kuomba kura za ushindi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wote wa CCM.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za ubunge na udiwani wilayani Kilolo, Tendega alisema ni wajibu wa wanaCCM wote kushirikiana kikamilifu kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

“Lazima tuungane kusaka kura za Rais, wabunge na madiwani. Kazi kubwa aliyoifanya Rais wetu mnaijua. Chama chochote cha siasa kinapogombea lengo lake ni kushika dola. Sasa wale wengine wanaoweka mpira kwapani waambieni kuwa Chama Cha Mapinduzi tunakwenda kutiki kwa wagombea wote wa CCM na kuleta kura za heshima,” alisema Tendega.

Aidha, aliongeza kuwa Rais Dkt. Samia ameahidi huduma za afya bure kwa wazee, watoto na watu wenye ulemavu kwa siku 100 za mwanzo wa uongozi wake.

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Kilolo, Dkt. Ritha Kabati, alisema ataendeleza miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Justine Nyomoga, pamoja na kutekeleza miradi yote iliyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Nazijua changamoto zote za Mkoa wa Iringa, ikiwemo Wilaya ya Kilolo. Siendi kuanza upya, nitaendeleza pale alipoishia Mbunge aliyepita kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinatatuliwa,” alisema Kabati.

Aliongeza kuwa Ilani ya CCM imeweka kipaumbele katika miundombinu, elimu na sekta mbalimbali, na akaahidi kutenda haki bungeni kwa kusimamia utekelezaji wake.

“Kilolo ni jimbo kubwa lenye kata nyingi. Tunapaswa kuepuka makundi na ubaguzi, badala yake tushirikiane kwa ajili ya maendeleo. Jimbo hili lina utajiri mkubwa unaoweza kuinua maisha ya wananchi wake tukishirikiana kwa mshikamano,” alisema Kabati.

Mratibu wa Uchaguzi wa CCM Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, Salim Abri Asas, alizindua rasmi kampeni hizo na kuwataka wananchi kumpigia kura za ndiyo Dkt. Kabati pamoja na madiwani wote wa CCM.

“hakuna sababu ya kutomchagua hakuna. Kwa mara ya kwanza tumepata mgombea mwanamke mwenye moyo wa kujali wananchi. Si mgeni kwenye nafasi ya ubunge, na atakapoingia bungeni ataanza mara moja na jimbo la Kilolo. Hakuna sababu ya kutompa kura Dkt. Kabati,” alisema Asas.

Aliyekuwa Mbunge wa Kilolo, Justine Nyomoga, alisema uzinduzi huo ni mwanzo wa safari ya kisiasa ya Dkt. Kabati na madiwani wa CCM, akisisitiza kuwa ataunga mkono kikamilifu kampeni za chama hicho.

“Namuunga mkono mgombea ubunge pamoja na madiwani wote. Nitashiriki kikamilifu katika kampeni kuhakikisha kura za ndiyo zinapatikana kwa Rais Dkt. Samia, Mbunge na madiwani wote wa CCM,” alisema Nyomoga.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI