Header Ads Widget

MTENDAJI MKUU UCSAF - 'WANANCHI TUMIENI MITANDAO YA MAWASILIANO VIZURI'


Na Lilian Kasenene,Morogoro

Matukio Daima Media. 

MTENDAJI Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF) mhandisi Peter Mwasyalanda amehimiza wananchi wa Kijiji cha Msolokelo kata ya Pemba Wilayani Mvomero,kutumia vyema mitandao ya mawasiliano kwa kujijenga kiuchumi, kielimu na kijamii.

Alisema hayo kijijini hapo baada ya kuzinduliwa Rasmi kwa mnara wa mawasiliano, na kuzungumza na wananchi ambapo  uzinduzi wa mnara huo wa mawasiliano uliojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom alieleza kuwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Serikali Desemba 03 mwaka Jana.

Mtendaji huyo mkuu alisema ahadi hiyo ilitolewa baada ya Waziri wa Masiliano, Jerry Slaa na Timu ya wataalam kutoka Mfuko huo kutembelea kijijini hapo na kushuhudia changamoto kubwa ya ukosefu wa mawasiliano ya simu ambapo wananchi walilazimika kutumia eneo Moja walilolibatiza kwa jina la "Mawasiliano" kupata huduma hiyo kwa shida.

"Serikali ya awamu ya sita haina Mchezo, ikiahidi inatekeleza,hapa tuliambiwa hata kabla nchi ya Tanzania haijaanzishwa hakukuwahi kuwa na mawasiliano,lakini Serikali imesikia kilio chenu na ndani ya kipindi kifupi mmepata, naona vijana hata simu za kupangusa wanazo na wanazitumia tangu Agosti mnara ulipowashwa,"alisema Mtendaji Mkuu wa UCSAF.

Akasema kupitia mradi wa Ujenzi wa minara, tayari minara 758 imejengwa kwenye maeneo yaliyokuwa na changamoto ya mtandao wa mawasiliano na nia ya Serikali ni kuhakikisha maeneo yote yenye changamoto hiyo yanafikiwa.

Mhandisi Masalyanga akawahimiza wananchi kutumia vizuri mitandao ya mawasiliano kupata maendeleo yakiwemo ya Kiuchumi, kijamii na kielimu na Mikakati ya Serikali kwa sasa ni kukuza uchumi kwa njia ya kidijitali.

"Mnaweza kutumia simu zenu kupata taarifa za masoko ya Mazao ya biashara na kilimo, mkafahamu Bei za mbolea, pembejeo,mbegu na mkaagizia kupitia mitandao ya simu na mkaletewa badala ya kuhangaika na kutumia muda mwingi kuzifuata wenyewe, "aliongeza Mtendaji Mkuu huyo wa UCSAF 

Mapema Mwenyekiti wa Kijiji cha Msolokelo Bw Hamis Gebo alisema uzinduzi wa mnara huo umekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi kwani awali walipata changamoto nyingi ikiwemo watumishi wanaopelekwa kikazi kijijini hapo kuomba uhamisho ama kuondoka kutokana na kukosa mawasiliano kabisa.

"Msolokelo tulikuwa kama tuko kaburini, lakini sasa mmeturudisha duniani, tunamshukuru sana Rais wetu (Mhe Samia Suluhu Hassan) kwa kusikia kilio chetu na kuwatuma mshughulikie kwa haraka, hakika yeye ni Kiongozi bora anayejali maisha ya Watanzania,Leo tumerudi duniani, shida imekwisha,"alisema Mwenyekiti huyo.

Baadhi ya wananchi Hassan Adam Mohamed, Rehema Gervas, Tabu Famau na Mathias Carol walisema awali wananchi walilazimika kupanda kwenye eneo Moja tu katika mlima wa Lunyasi, Umbali mrefu kutoka kwenye makazi kutafuta mawasiliano, ama juu ya mti mmoja maarufu kijijini hapo, Hali ambayo haikuwa salama wanapopata dharura usiku kama ugonjwa ama huduma za uzazi kwa wanawake.

"Mfano una mke amepata dharura ya kujifungua usiku, unakosa msaada wa haraka, jambo ambalo ni hatari kwa Mama na Mtoto, tunashukuru sasa muda wowote tunapiga simu, mwanzo ilikuwa ni lazima uende Milimani ama upande kwenye ule mti mmoja tu kubahatisha mawasiliano ya Halotel au Airtel, tunashukuru sana Serikali,"aliongeza Adam Mohamed.

Msimamizi wa UCSAF Kanda ya Mashariki Baraka Eliezer alisema awali Waziri wa Mawasiliano Jerry Slaa walifika kijijini hapo Desemba 03, 2024,na kukutana na hali mbaya ya mawasiliano kijijini hapo lakini baada ya kuwashwa mnara wananchi wanawasha simu zilizokuwa zinazimwa.

Kijiji cha Msolokelo kina wakazi takribani 16,801 na bado Kijiji jirani cha Gonja kinahitaji huduma ya mawasiliano kutokana na kuwa na kero iliyofanana na ilivyokuwa kwenye Kijiji cha Msolokelo kabla ya kuzinduliwa kwa mnara wa mawasiliano.

Mwisho.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI