Moshi. Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, ameahidi kushughulikia kwa vitendo suala la Manispaa ya Moshi kupandishwa hadhi kuwa jiji endapo atapata ridhaa ya wananchi kuwa mbunge.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni, Shayo amesema suala la Moshi kuwa jiji limekuwa changamoto kubwa kwa miaka mingi, lakini akasisitiza kuwa atalisimamia kwa nguvu zote hadi kufanikishwa.
"Ndugu zangu lipo suala kubwa sana na huu mfupa umewashinda watu wengi, ukiangalia Tanga ni jiji, Arusha ni jiji lakini Moshi siyo jiji, nitakwenda kukaa na mbunge wa Moshi vijijini nitengeneze hoja ya upanuzi wa huu mji, haiwezekani wageni wanakuja kutoka ulaya kwa ajili ya utalii halafu wanashuka Manispaa, sasa tunataka wakija washuke katika jiji la moshi, nipeni kura za kutosha na mpeni Rais Samia kura za kutosha".
Mbali na hilo, ameahidi kusimamia ujenzi wa stendi ya kimataifa ya Ngangamfumuni, akisema ndani ya miaka miwili hadi mitatu stendi hiyo itakuwa imekamilika na kuwa historia ya maendeleo kwa wakazi wa Moshi
Vipaumbele vingine alivyoahidi Shayo ni kuimarisha ukusanyaji na usafirishaji wa taka kwa kupata magari mapya,kujenga barabara za pembezoni kwa kiwango cha lami pamoja na kufufua na kujenga viwanda vipya ili kuinua uchumi wa wananchi.
"Lakini pia nitaishauri Serikali kujenga shule za ghorofa kutokana na ufinyu wa ardhi mjini Moshi, Kusimamia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kufika kwa walengwa wote na kuandaa mashindano ya mara kwa mara ya wasanii ili kukuza vipaji" amesema Shayo.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Namelok Sokoine, amewataka wakazi wa Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kumpigia kura Rais Samia Suluhu Hassan, wagombea ubunge na madiwani wote wa CCM.
Alisema Serikali ya awamu ya sita imetoa zaidi ya Sh1.4 Trilion kwa ajili ya miradi ya maendeleo mkoani humo, hatua iliyoleta mageuzi makubwa katika sekta za elimu, afya na miundombinu.
“Tutasaka kura kata kwa kata, mtaa kwa mtaa na kitanda kwa kitanda. Ni wajibu wetu kumpa Rais Samia kura nyingi kama shukrani kwa maendeleo makubwa yaliyotekelezwa mkoani Kilimanjaro".
0 Comments